1 Chronicles 10

Sauli Ajiua

Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, wengi wakauawa katika mlima Gilboa. Wafilisti wakawafuatia kwa bidii Sauli na wanawe, wakawaua wanawe Yonathani, Abinadabu na Malki-Shua. Mapigano yakawa makali kumzunguka Sauli na wakati wapiga mishale walipompata, wakamjeruhi.

Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watanidhalilisha.”

Lakini yule mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuthubutu kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake akajichoma mwenyewe.
Mbeba silaha wake alipoona kwamba Sauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake akafa. Kwa hiyo Sauli na wanawe watatu wakafa, pamoja na nyumba yake yote.

Waisraeli wote waliokuwa bondeni walipoona kwamba jeshi limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, waliacha miji yao wakakimbia. Nao Wafilisti wakaja na kukaa humo.

Kesho yake, Wafilisti walipokuja kuchukua nyara za hao waliouawa, walimkuta Sauli na wanawe wameanguka juu ya Mlima Gilboa. Wakamvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, wakawatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari hizi miongoni mwa sanamu zao na watu wao. 10 Waliweka silaha zake katika hekalu la miungu yao, wakatundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.

11 Wakazi wote wa Yabeshi-Gileadi waliposikia hayo yote Wafilisti waliyomtendea Sauli, 12 mashujaa wote wakaondoka, wakautwaa mwili wa Sauli na miili ya wanawe, wakaileta Yabeshi. Wakaizika mifupa yao chini ya mti mkubwa huko Yabeshi, nao wakafunga kwa siku saba.

13 Sauli alikufa kwa sababu hakuwa mwaminifu kwa BWANA. Hakulishika neno la BWANA, hata akataka shauri kwa mwaguzi kwa ajili ya uongozi, 14 hakumwuliza BWANA. Kwa hiyo BWANA alimwua, na ufalme akampa Daudi mwana wa Yese.

Copyright information for Neno