1 Chronicles 13

Kurudishwa Kwa Sanduku La Mungu

Daudi alishauriana na kila afisa wake, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. Ndipo akaliambia kusanyiko lote la Israeli, “Kama mkiona ni vyema na kama ni mapenzi ya BWANA Mungu wetu, tupeleke ujumbe kwa ndugu zetu wengine walio mbali na walio karibu katika nchi yote ya Israeli, pia kwa makuhani na Walawi walio pamoja nao katika miji yao na katika sehemu zao za malisho yao waje waungane na sisi. Sisi na tulirudishe Sanduku la Mungu wetu kwetu kwa maana hatukujali wakati wa utawala wa Sauli.” Kusanyiko lote likakubaliana kufanya hivyo, kwa sababu ilionekana vyema kwa watu wote.

Basi Daudi akawakusanya Waisraeli wote, kuanzia Mto Shihori ulioko Misri hadi Lebo-Hamathi, ili kulileta Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu. Daudi akiwa pamoja na Waisraeli wote wakaenda Baada ya Yuda (Kiriath-Yearimu) kulipandisha Sanduku la Mungu BWANA kutoka huko, ambaye anaketi katika kiti chake cha enzi kilichoko kati ya makerubi, sanduku ambalo linaitwa kwa Jina lake.

Wakalisafirisha Sanduku la Mungu kwa gari jipya lenye magurudumu mawili likikokotwa na maksai kutoka katika nyumba ya Abinadabu, Uza na Ahio wakiliongoza gari hilo. Daudi pamoja na Waisraeli wote walikuwa wanasifu kwa nguvu zao zote mbele za Mungu, kwa nyimbo na kwa vinubi, zeze, matari, matoazi na tarumbeta.

Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza akaunyosha mkono wake ili kulizuia Sanduku, kwa sababu hao maksai walijikwaa. 10 Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Uza, akampiga kwa sababu aliuweka mkono wake kwenye Sanduku. Kwa hiyo akafa pale mbele za Mungu.

11 Kisha Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya BWANA iliwaka dhidi ya Uza, mahali pale pakaitwa Peres-Uza
13.11 Maana yake ni Gadhabu dhidi ya Uza
hadi leo.

12 Siku ile Daudi akamwogopa Mungu naye akauliza. “Nitawezaje kulichukua Sanduku la Mungu kwangu?” 13 Hakulichukua hilo Sanduku akae nalo katika Mji wa Daudi. Badala yake, akalipeleka nyumbani kwa Obed-Edomu, Mgiti. 14 Sanduku la Mungu likabaki pamoja na jamaa ya Obed-Edomu, nyumbani kwake, kwa miezi mitatu, naye BWANA akaibariki nyumba yake pamoja na kila kitu alichokuwa nacho.

Copyright information for Neno