1 Chronicles 16

Sanduku Lawekwa Ndani Ya Hema

1Wakaleta Sanduku la Mungu na kuliweka ndani ya hema ambalo Daudi alikuwa amelisimamisha kwa ajili hiyo, wakatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Mungu. 2Baada ya Daudi kutoa hizo sadaka za kuteketezwa na hizo sadaka za amani, akawabariki watu katika jina la BWANA. 3Kisha akamgawia kila Mwisraeli mwanaume na mwanamke mkate, maandazi ya tende na maandazi ya zabibu kavu.

4Akawaweka pia baadhi ya Walawi ili wahudumu mbele ya Sanduku la BWANA kufanya maombi, kumshukuru na kumsifu BWANA, Mungu wa Israeli: 5Asafu ndiye aliyekuwa mkuu wao, akisaidiwa na Zekaria, Yeieli, Shemiramothi, Yehieli, Matithia, Eliyabu, Benaya, Obed-Edomu na Yeieli. Hawa ndio ambao wangepiga zeze na vinubi, Asafu angelipiga matoazi, 6nao Benaya na Yahazieli makuhani, ndio ambao wangelipiga tarumbeta mara kwa mara mbele ya Sanduku la Agano la Mungu.

Zaburi Ya Daudi Ya Shukrani

7Siku ile kitu cha kwanza Daudi alichofanya ni kumkabidhi Asafu na wenzake zaburi hii ya shukrani kwa BWANA: 8Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake,
wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
9Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa,
waambieni matendo yake yote ya ajabu.
10Utukufu kwa jina lake takatifu,
mioyo ya wale wamtafutao BWANA na ifurahi.
11Mtafuteni BWANA na nguvu zake,
utafuteni uso wake siku zote.
12Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya,
miujiza yake na hukumu alizozitamka.
13Ee wazao wa Israeli mtumishi wake,
Ee wana wa Yakobo, wateule wake.
14Yeye ndiye BWANA Mungu wetu,
hukumu zake zimo duniani pote.
15Hulikumbuka Agano lake milele,
neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
16Agano alilolifanya na Abrahamu,
kiapo alichomwapia Isaki.
17Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri,
kwa Israeli kuwa Agano la milele:
18“Wewe nitakupa nchi ya Kanaani
kuwa sehemu utakayoirithi.”
19Walipokuwa wachache kwa idadi,
wachache sana na wageni ndani yake,
20walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine,
kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
21Hakuruhusu mtu ye yote awaonee,
kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema,
22“Msiwaguse masiya
16.22 Maana yake Aliyetiwa mafuta
wangu,
msiwadhuru manabii wangu.”
23Mwimbieni BWANA dunia yote;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
24Tangazeni utukufu wake katikati ya mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
25Kwa kuwa BWANA ni mkuu,
mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote,
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
26Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini BWANA aliziumba mbingu.
27Fahari na enzi viko mbele yake,
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
28Mpeni BWANA, enyi jamaa za mataifa,
mpeni BWANA utukufu na nguvu,
29mpeni BWANA utukufu
unaostahili jina lake.
Leteni sadaka na mje katika nyua zake;
mwabuduni BWANA katika uzuri
wa utakatifu wake,
30Dunia yote na itetemeke mbele zake.
Ulimwengu ameuweka imara;
hauwezi kusogezwa.
31Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
katikati ya mataifa semeni,
“BWANA anatawala.”
32Bahari na ivume na vyote vilivyomo ndani yake;
mashamba na yashangilie,
na vyote vilivyomo ndani yake.
33Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha,
itaimba mbele za BWANA
kwa maana anakuja kuihukumu dunia.
34Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni Mwema,
upendo wake wadumu milele.
35Mlilieni, “Ee Mungu Mwokozi wetu, tuokoe;
utukusanye tena kutoka katika mataifa,
ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,
na kujisifu katika sifa zako.”
36Atukuzwe BWANA, Mungu wa Israeli,
tangu milele na hata milele.Nao watu wote wakasema, “Amen,” na, “Msifuni BWANA.”37Daudi akamwacha Asafu na wenzake mbele ya Sanduku la Agano la BWANA ili wahudumu humo mara kwa mara, kulingana na mahitaji ya kila siku. 38Pia akamwacha Obed-Edomu pamoja na wenzake sitini na wanane wahudumu pamoja nao. Obed-Edomu mwana wa Yeduthuni na pia Hosa walikuwa mabawabu wa lango.

39Daudi akamwacha Sadoki, kuhani, pamoja na makuhani wenzake mbele ya hema ya ibada ya BWANA katika mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni 40ili kutoa sadaka za kuteketezwa kwa BWANA kwenye madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa mara kwa mara, asubuhi na jioni, sawasawa na kila kitu kilichoandikwa katika sheria ya BWANA ambayo alikuwa amempa Israeli. 41Waliohudumu pamoja nao walikuwa Hemani, Yeduthuni na wale wote waliochaguliwa na kutajwa kwa jina kumpa BWANA shukrani, “Kwa maana fadhili zake zadumu milele.” 42Hemani na Yeduthuni walikuwa na wajibu wa kupiga tarumbeta, matoazi na kutumia vyombo vingine kwa ajili ya nyimbo za sifa kwa Mungu. Wana wa Yeduthuni waliwekwa langoni.

43Kisha watu wote wakaondoka, kila mmoja akarudi nyumbani kwake, naye Daudi akarudi nyumbani kuibariki jamaa yake.

Copyright information for Neno