1 Chronicles 17

Ahadi Ya Mungu Kwa Daudi

Baada ya Daudi kukaa kwa utulivu katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mierezi, wakati Sanduku la Agano la BWANA liko ndani ya hema.”

Nathani akamjibu Daudi, “Lo lote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa sababu Mungu yuko pamoja na wewe.” Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema:

“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, hili ndilo asemalo BWANA, ‘Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo. Mimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku ile niliyowatoa Israeli kutoka Misri mpaka leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine na kutoka mahali pamoja hadi pengine. Je, po pote nilipokwenda pamoja na Waisraeli wote, wakati wo wote nilimwambia kiongozi ye yote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?’ ”

“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo BWANA Mwenye Nguvu Zote: Nilikuchukua machungani na kutoka kuandama kondoo ili uwatawale watu wangu Israeli. Nimekuwa pamoja nawe po pote ulipokwenda, nami nimewakatilia mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kama majina ya watu wengine wakuu sana wa dunia. Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya hapo mwanzo, 10 na ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote.

“ ‘Pamoja na hayo ninakuambia kwamba BWANA atakujengea nyumba:
11 Wakati wako utakapokuwa umekwisha, nawe ukawa umekwenda kukaa na baba zako, nitamwinua mzao wako aingie mahali pako kuwa mfalme, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitaufanya imara ufalme wake. 12 Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakifanya imara kiti cha ufalme wake milele. 13 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yeye aliyekutangulia. 14 Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele, kiti chake cha enzi nitakifanya imara milele.’ ”15 Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

Maombi Ya Daudi

16 Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani akaketi mbele za BWANA akasema:

“Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu na jamaa yangu ni nini, hata unitendee haya yote?
17 Kama vile haya hayakutosha machoni pako, Ee Mungu, umesema pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukukakuliko watu wote, Ee BWANA Mungu.

18 “Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako, 19 Ee BWANA Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa sana na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kubwa sana.

20 “Hakuna aliye kama wewe, Ee BWANA Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe. 21 Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa moja duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, wa kufanya maajabu makubwa ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, uliowakomboa kutoka Misri? 22 Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA Mungu, umekuwa Mungu wao.

23 “Sasa basi, BWANA ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi, 24 ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako.

25 “Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea yeye nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya. 26 Ee BWANA, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri. 27 Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili ipate kudumu milele machoni pako, kwa ajili yako, Ee BWANA, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”

Copyright information for Neno