1 Chronicles 18

Ushindi Wa Daudi

1Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, akautwaa Gathi pamoja na vijiji vinavyouzunguka kutoka katika utawala wa Wafilisti.

2Daudi akawashinda pia Wamoabu, wakawa watumishi wake, nao wakawa wanamletea ushuru.

3Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mfalme wa Soba, hadi Hamathi, wakati alipokwenda kuimarisha utawala wake katika Mto Eufrati. 4Daudi akateka magari ya vita 1,000 miongoni mwa magari yake, waendesha hayo magari ya kukokotwa na farasi 7,000 na askari wa miguu 20,000. Daudi akakata mishipa ya miguu ya nyuma ya farasi wote wakokotao magari, ila akabakiza 100.

5Waaramu wa Dameski, walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao. 6Kisha Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski. Basi Waaramu wakawa watumishi wa Daudi, wakawa wanamletea ushuru. BWANA akampa Daudi ushindi kila mahali alipokwenda.

7Daudi akatwaa zile ngao za dhahabu zilizochukuliwa na maafisa wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu. 8Kutoka mji wa Tibhathi na mji wa Kuni, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Daudi akachukua pia shaba nyingi sana, ambayo Solomoni aliitumia kutengenezea ile Bahari ya shaba, zile nguzo na vifaa mbalimbali vya shaba.

9Tou mfalme wa Hamathi aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri mfalme wa Soba, 10akamtuma mwanawe, Hadoramu kwa Mfalme Daudi ili kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake juu ya Mfalme Hadadezeri vitani, kwa kuwa alikuwa amepigana vita mara nyingi na Tou. Hadoramu akamletea Daudi vifaa mbalimbali vya dhahabu fedha na shaba.

11Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa BWANA kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu aliyokuwa ameitwaa katika mataifa yote haya: Edomu na Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki.

12Abishai mwana wa Seruya akawaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi. 13Akaweka askari walinzi huko Edomu, nao Waedomu wote wakawa watumishi wa Daudi. BWANA akampa Daudi ushindi kila mahali alipokwenda.

Maafisa Wa Daudi

14Daudi akatawala katika Israeli yote, akitenda lililo haki na lililo sawa kwa watu wake wote. 15Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa mkuu wa jeshi, Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mtunza kumbukumbu, 16Sadoki, mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani, Shavsha alikuwa mwandishi, 17naye Benaya, mwana wa Yehoyada alisimamia Wakerethi na Wapelethi, nao wana wa Daudi walikuwa maafisa wakuu katika utumishi wa mfalme.

Copyright information for Neno