1 Chronicles 11

Daudi Atiwa Mafuta Kuwa Mfalme Wa Israeli

1Israeli yote walimjia Daudi kwa pamoja huko Hebroni wakamwambia, “Sisi ni nyama yako na damu yako. 2Wakati wote uliopita, hata wakati Sauli alipokuwa mfalme, wewe ndiwe uliyeiongoza Israeli vitani, naye BWANA Mungu wako alikuambia, ‘Wewe utawachunga watu wangu Israeli, na utakuwa mtawala wao.’ ”

3Wazee wote wa Israeli walipokuwa wamewasili kwa Mfalme Daudi huko Hebroni, alifanya mapatano nao huko Hebroni mbele za BWANA, nao wakamtia Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli, sawasawa na BWANA alivyoahidi kupitia kwa Samweli.

Daudi Ashinda Yerusalemu

4Daudi na Waisraeli wote wakaenda Yerusalemu (ndio Yebusi). Nao Wayebusi, ambao ndio waliokuwa wanaishi humo 5wakamwambia Daudi, “Wewe hutaingia humu.” Hata hivyo, Daudi akaiteka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.

6Daudi alikuwa amesema, “Ye yote aongozaye mashambulizi dhidi ya Wayebusi, atakuwa jemadari mkuu.” Yoabu mwana wa Seruya, akawa wa kwanza kukwea, naye akawa mkuu.

7Daudi akafanya maskani yake kwenye ngome, hivyo ukaitwa Mji wa Daudi. 8Akajenga mji pande zote, kuanzia kwenye mito hadi kwenye ukuta kuzunguka, wakati huo huo Yoabu akajenga sehemu zingine zilizobaki za Yerusalemu. 9Daudi akazidi kuwa na nguvu zaidi na zaidi, kwa sababu BWANA Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.

Mashujaa Wa Daudi

10Hawa ndio waliokuwa wakuu wa mashujaa wa Daudi: wao pamoja na Israeli wote, wakauimarisha ufalme wake ili kuenea katika nchi yote, kama BWANA alivyoahidi. 11Hii ndio orodha ya mashujaa wa Daudi:

Yashobeamu, Mhakmoni, alikuwa mkuu wa maafisa; yeye aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300, ambao aliwaua katika pambano moja.

12Aliyefuata alikuwa Eleazari, mwana wa Dodai, Mwahohi, mmojawapo wa wale mashujaa watatu. 13Huyo alikuwa pamoja na Daudi huko Pas-Damimu, wakati Wafilisti walipokusanyika huko kwa ajili ya vita. Huko ambapo kulikuwa na shamba lililokuwa limejaa shayiri, vikosi vya Israeli vikawakimbia Wafilisti. 14Lakini Eleazari na Daudi wakasimama imara katikati ya lile shamba, nao wakalishindania na wakawaua Wafilisti. Naye BWANA akawapa ushindi mkubwa.

15Wakuu watatu miongoni mwa wale thelathini, walimwendea Daudi katika mwamba huko kwenye pango la Adulamu, wakati kikosi cha Wafilisti kilikuwa kimepiga kambi kwenye Bonde la Warefai. 16Wakati ule Daudi alikuwa katika ngome na askari walinzi wa Wafilisti walikuwa katika mji wa Bethlehemu. 17Daudi alitamani maji akasema, “Laiti mtu angenipatia maji ya kunywa kutoka kisima kilichoko karibu na lango la Bethlehemu!” 18Kwa hivyo wale watatu, wakapita katikati ya safu za Wafilisti, wakachota maji kutoka kwenye hicho kisima kilichoko nje ya lango la Bethlehemu, wakamletea Daudi. Lakini yeye akakataa kuyanywa. Badala ya kuyanywa akayamimina mbele za BWANA. 19Akasema, “Mungu apishie mbali kwamba nifanye hivi! Je kweli, niinywe damu ya watu hawa waliohatarisha maisha yao?” Kwa sababu walihatarisha maisha yao kuyaleta yale maji, Daudi hakukubali kuyanywa.

Huo ndio uliokuwa ujasiri wa wale mashujaa watatu.

20Abishai, nduguye Yoabu alikuwa mkuu wa wale Watatu. Aliinua mkuki wake dhidi ya watu 300, ambao aliwaua, hivyo akawa maarufu kama wale Watatu. 21Alitunukiwa heshima maradufu ya wale Watatu, akawa jemadari wao, ingawa hakuhesabiwa miongoni mwao.

22Benaya, mwana wa Yehoyada alikuwa mpiganaji hodari kutoka Kabseeli, aliyefanya mambo makubwa ya ujasiri. Aliwaua watu wawili mashujaa wa Moabu. Pia aliingia shimoni siku ya theluji na kumwua simba. 23Alimwua Mmisri aliyekuwa na urefu kama dhiraa tano
11.23 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25
. Ingawa Mmisri alikuwa na mkuki kama mti wa mfumaji mkononi mwake, Benaya alimwendea na rungu. Akamnyang'anya Mmisri mkuki wake na kumwua nao.
24Mambo kama hayo ya ujasiri ndiyo aliyoyafanya Benaya, mwana wa Yehoyada, yeye pia alikuwa maarufu kama wale mashujaa watatu. 25Yeye aliheshimiwa zaidi ya wale Thelathini, lakini hakujumuishwa miongoni mwa wale Watatu: Daudi akamweka kuwa kiongozi wa kundi la walinzi wake. 26

  • Wale watu mashujaa walikuwa:
  • Asaheli nduguye Yoabu,
  • Ehanani mwana wa Dodo kutoka Bethlehemu,
27Shamothi, Mharori, Helesi, Mpeloni, 28Ira mwana wa Ikeshi kutoka Tekoa, Abiezeri kutoka Anathothi, 29Sibekai, Mhushathi, Ilai, Mwahohi, 30Maharai, Mnetofathi, Heledi mwana wa Baana, Mnetofathi, 31Itai mwana wa Ribai kutoka Gibea ya Benyamini, Benaya, Mpirathoni, 32Hurai kutoka mabonde ya Gaashi, Abieli, Mwairibathi, 33Azmawethi, Mbaharumi, Eliyahba, Mshaalboni, 34wana wa Hashemu, Mgiloni, Yonathani mwana wa Shagee, Mharari, 35Ahiamu mwana wa Sakari, Mharari, Elifale mwana wa Uri, 36Heferi, Mmekerathi, Ahia, Mpeloni, 37Hezro, Mkarmeli, Naarai mwana wa Ezbai. 38Yoeli nduguye Nathani, Mibhari mwana wa Hagri, 39Seleki, Mwamoni, Naharai, Mbeorothi, mbeba silaha wa Yoabu mwana wa Seruya, 40Ira, Muithiri, Garebu, Muithiri, 41Uria, Mhiti, Zabadi mwana wa Ahlai, 42Adina mwana wa Shiza, Mreubeni, ambaye alikuwa mkuu wa Wareubeni, akiwa pamoja na watu thelathini, 43Hanani mwana wa Maaka, Yoshafati, Mmithni, 44Uzia, Mwashterathi, Shama na Yeieli wana wa Hothamu, Mwaroeri, 45Yediaeli mwana wa Shimri, nduguye Yoha, Mtizi, 46Elieli, Mmahawi, Yeribai na Yoshavia wana wa Elnaamu, Ithma, Mmoabi, 47Elieli, na Obedi na Yaasieli, Mmesobai.
Copyright information for Neno