1 Corinthians 15

Kufufuka Kwa Kristo

Basi ndugu zangu nataka niwakumbushe kuhusu Injili niliyowahubiria, mkaipokea na ambayo katika hiyo mmesimama. Kwa Injili hii mnaokolewa mkishikilia kwa uthabiti neno nililowahubiria ninyi. La sivyo, mmeamini katika ubatili.

Kwa maana yale niliyopokea ndiyo niliyowapa ninyi, kama yenye umuhimu wa kwanza: Kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yasemayo Maandiko, ya kuwa alizikwa na alifufuka siku ya tatu, na kwamba alimtokea Kefa
15:5 Yaani Petro
, kisha akawatokea wale kumi na wawili.
Baadaye akawatokea wale ndugu waamini zaidi ya 500 kwa pamoja, ambao wengi wao bado wako hai, ingawa wengine wamelala. Ndipo akamtokea Yakobo na kisha mitume wote. Mwisho wa wote, akanitokea mimi pia, ambaye ni kama aliyezaliwa si kwa wakati wake.

Kwa maana mimi ndiye mdogo kuliko mitume wote, nisiyestahili kuitwa mtume, kwa sababu nililitesa kanisa la Mungu. 10 Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo na neema yake kwangu haikuwa kitu bure. Bali nilizidi sana kufanya kazi kuliko mitume wote, lakini haikuwa mimi, bali ni ile neema ya Mungu iliyokuwa pamoja nami. 11 Hivyo basi, kama ilikuwa ni mimi au ni wao hili ndilo tulihubirilo na hili ndilo mliaminilo.

Ufufuo Wa Wafu

12 Basi kama tumehubiri ya kwamba Kristo alifufuka kutoka kwa wafu, mbona baadhi yenu mnasema hakuna ufufuo wa wafu? 13 Lakini kama hakuna ufufuo wa wafu, basi hata Kristo hakufufuka. 14 Tena ikiwa Kristo hakufufuka kutoka kwa wafu, kuhubiri kwetu kumekuwa ni bure na imani yenu ni batili. 15 Zaidi ya hayo basi, twaonekana kuwa mashahidi wa uongo wa Mungu, kwa sababu tumeshuhudia kumhusu Mungu kwamba alimfufua Kristo kutoka kwa wafu, lakini hilo haliwezi kuwa kweli kama wafu hawafufuliwi. 16 Kwa kuwa kama wafu hawafufuliwi, basi hata Kristo hajafufuka. 17 Tena kama Kristo hajafufuka, imani yenu ni batili, nanyi bado mko katika dhambi zenu. 18 Hivyo basi, wote waliolala katika Kristo wamepotea. 19 Ikiwa tumaini letu ndani ya Kristo ni kwa ajili ya maisha haya tu, sisi tunastahili kuhurumiwa kuliko watu wengine wote duniani.

20 Lakini kweli Kristo amefufuka kutoka kwa wafu, tunda la kwanza la wale wote waliolala. 21 Kwa maana kama vile mauti ilivyokuja kwa njia ya mtu mmoja, vivyo hivyo, ufufuo wa wafu umekuja kwa njia ya mtu mmoja. 22 Kwa maana kama vile katika Adamu watu wote wanakufa, vivyo hivyo katika Kristo wote watafanywa hai. 23 Lakini kila mmoja kwa wakati wake: Kristo, tunda la kwanza la ufufuo, kisha, wale walio wake, wakati atakapokuja. 24 Ndipo mwisho utafika, wakati atakapomkabidhi Mungu Baba Ufalme, akiisha angamiza kila utawala na kila mamlaka na nguvu. 25 Kwa maana lazima Kristo atawale mpaka awe amewaweka adui zake wote chini ya miguu yake. 26 Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni mauti. 27 Kwa maana Mungu “ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini isemapo kwamba “vitu vyote” vimewekwa chini yake, ni wazi kwamba Mungu aliyetiisha vitu vyote chini ya Kristo hayumo miongoni mwa hivyo vilivyotiishwa. 28 Atakapokuwa amekwisha kutiisha vitu vyote chini ya Mwana, ndipo Mwana mwenyewe atatiishwa chini yake yeye aliyetiisha vitu vyote, ili Mungu awe yote katika yote.

29 Basi kama hakuna ufufuo, watafanyaje wale wabatizwao kwa ajili ya wafu? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, mbona watu wanabatizwa kwa ajili yao? 30 Nasi kwa upande wetu kwa nini tunajihatarisha kila saa? 31 Kama majivuno yangu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu Bwana wetu ni kweli, ndugu zangu, ninakufa kila siku. 32 Kama kwa tumaini la kibinadamu tu nilipigana na wanyama wakali huko Efeso, ningekuwa nimepata faida gani kwa jambo hilo? Kama wafu hawafufuliwi, “Sisi na tule na kunywa,
kwa kuwa kesho tutakufa.”


33 Msidanganyike: “Ushirika na watu wabaya huharibu tabia njema.” 34 Zindukeni mwe na akili kama iwapasavyo, msitende dhambi tena; kwa maana watu wengine hawamjui Mungu. Nasema mambo haya ili mwone aibu.

Mwili Wa Ufufuo

35 Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” 36 Ninyi wapumbavu! Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. 37 Mpandapo, hampandi mwili ule unaotegemewa kuwako, bali mwapanda mbegu tupu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. 38 Lakini Mungu huipa hiyo mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. 39 Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. 40 Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini uzuri wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na uzuri wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine. 41 Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.

42 Hivyo ndivyo itakavyokuwa wakati wa ufufuo wa wafu. Ule mwili wa kuharibika uliopandwa, utafufuliwa usioharibika, 43 unapandwa katika aibu, unafufuliwa katika utukufu, unapandwa katika udhaifu, unafufuliwa katika nguvu, 44 unapandwa mwili wa asili, unafufuliwa mwili wa kiroho.

Kama kuna mwili wa asili, basi kuna mwili wa kiroho pia.
45 Kwa hiyo imeandikwa, “Mtu wa kwanza Adamu alifanyika kiumbe hai”; Adamu wa mwisho, yeye ni roho iletayo uzima. 46 Lakini si ule wa kiroho uliotangulia, bali ni ule wa asili, kisha ule wa kiroho. 47 Mtu wa kwanza aliumbwa kwa mavumbi ya ardhini, mtu wa pili alitoka mbinguni. 48 Kama vile alivyokuwa yule wa ardhini, ndivyo walivyo wale walio wa ardhini; na kwa vile alivyo mtu yule aliyetoka mbinguni, ndivyo walivyo wale walio wa mbinguni. 49 Kama vile tulivyochukua mfano wa yule mtu wa ardhini, ndivyo tutakavyochukua mfano wa yule mtu aliyetoka mbinguni.

50 Ndugu zangu nisemalo ni hili: nyama na damu haviwezi kuurithi Ufalme wa Mungu, wala kuharibika kurithi kutokuharibika. 51 Sikilizeni, nawaambia siri: Sote hatutalala, lakini sote tutabadilishwa 52 ghafula, kufumba na kufumbua, parapanda ya mwisho itakapolia. Kwa kuwa parapanda italia, nao wafu watafufuliwa na miili isiyoharibika, nasi tutabadilishwa. 53 Kwa maana mwili huu wa kuharibika lazima uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa lazima uvae kutokufa. 54 Kwa hiyo, mwili huu wa kuharibika utakapovaa kutokuharibika, nao huu mwili wa kufa utakapovaa kutokufa, ndipo lile neno lililoandikwa litakapotimia: “Mauti imemezwa kwa kushinda.” 55 “Kuko wapi, Ewe mauti, kushinda kwako?
Uko wapi, Ewe mauti, uchungu wako?”


56 Uchungu wa mauti ni dhambi na nguvu ya dhambi ni sheria. 57 Lakini ashukuriwe Mungu, yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

58 Kwa hiyo, ndugu zangu wapenzi, simameni imara, msitikisike, mzidi sana katika kuitenda kazi ya Bwana, kwa maana mnajua ya kuwa, kazi yenu si bure katika Bwana.

Copyright information for Neno