1 Corinthians 2

Kumtangaza Kristo Aliyesulibiwa

1Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu. 2Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu cho chote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo, naye amesulibiwa msalabani. 3Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana. 4Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya kuwashawishi watu, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho Mtakatifu 5ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

Hekima Ya Kweli Itokayo Kwa Mungu

6Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika. 7Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika kwa wanadamu, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu. 8Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati zetu aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulibisha Bwana wa utukufu. 9Lakini ni kama ilivyoandikwa: “Lile jambo ambalo jicho halijapata kuona,
sikio halijapata kusikia,
wala halikuingia moyoni,
lile ambalo Mungu aliwaandalia
wale wampendao”:


10Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa njia ya Roho wake.

Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu.
11Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu. 12Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho yule atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure. 13Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa wale watu wa kiroho. 14Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa jinsi ya rohoni. 15Mtu wa kiroho hutambua mambo yote, lakini yeye mwenyewe hatambuliwi na mtu ye yote. 16“Kwa maana ni nani aliyejua nia ya Bwana
ili apate kumfundisha?”


Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.

Copyright information for Neno