1 John 1

Neno La Uzima

1Tunawajulisha lile lililokuwako tangu mwanzo, lile tulilosikia, ambalo tumeliona kwa macho yetu, ambalo tumelitazama na kuligusa kwa mikono yetu, kuhusu Neno la uzima. 2Uzima huo ulidhihirishwa; nasi tumeuona na kuushuhudia, nasi twawatangazia uzima wa milele, ambao ulikuwa pamoja na Baba, nao ukadhihirishwa kwetu. 3Twawatangazia lile tuliloliona na kulisikia, ili kwamba nanyi mwe na ushirika nasi. Na ushirika wetu hasa ni pamoja na Baba na Mwanawe, Yesu Kristo. 4Tunaandika mambo haya ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.

Kutembea Nuruni

5Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lo lote. 6Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli. 7Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake yatusafisha dhambi yote.

8Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. 9Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha toka kwenye udhalimu wote. 10Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

Copyright information for Neno