1 Kings 8

Sanduku La Agano Laletwa Hekaluni

Kisha Mfalme Solomoni akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la BWANA kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Solomoni wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.

Viongozi wote wa Israeli walipokwisha kufika, makuhani wakajitwika hilo Sanduku la Agano, wakalipandisha Sanduku la BWANA, Hema la Kukutania pamoja na vyombo vyote vitakatifu ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba, naye Mfalme Solomoni pamoja na kusanyiko lote la Israeli waliokusanyika kumzunguka walikuwa mbele ya hilo Sanduku, wakatoa dhabihu nyingi za kondoo na ng'ombe ambao idadi yao haikuwezekana kuandikwa au kuhesabiwa.

Ndipo makuhani wakalileta Sanduku la Agano la BWANA mahali pake ndani ya Hekalu, katika Patakatifu pa Patakatifu na kuliweka chini ya mabawa ya yale makerubi. Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea. Mipiko hiyo ilikuwa mirefu kiasi kwamba ncha zake ziliweza kuonekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya mahali Patakatifu pa Patakatifu, lakini si kutoka nje ya Mahali Patakatifu, nayo iko huko hadi leo. Hapakuwa na cho chote ndani ya Sanduku la Agano isipokuwa zile mbao mbili za mawe ambazo ziliwekwa na Mose huko Horebu, mahali ambapo BWANA alifanya Agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.

10 Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likalijaza Hekalu la BWANA. 11 Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa BWANA ulilijaza Hekalu lake.

12 Ndipo Solomoni akasema, “BWANA alisema kwamba ataishi katika giza nene; 13 naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.”

Hotuba Ya Solomoni

14 Kusanyiko lote la Israeli lilipokuwa limesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. 15 Kisha akasema:

“Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi baba yangu Daudi kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema,
16 ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lo lote la Israeli Hekalu lijengwe kwa ajili ya Jina langu ili lipate kuwako huko, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’

17 “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. 18 Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. 19 Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni nyama yako na damu yako mwenyewe, ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’

20 “BWANA ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile BWANA alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. 21 Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambamo ndani yake kuna Agano la BWANA lile alilofanya na baba zetu wakati alipowatoa Misri.”

Maombi Ya Solomoni Ya Kuweka Hekalu Wakfu

22 Kisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA machoni pa kusanyiko lote la Israeli, akakunjua mikono yake kuelekea mbinguni 23 na kusema:

“Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe mbinguni juu wala duniani chini, wewe unayetunza Agano lako la upendo pamoja na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.
24 Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.

25 “Sasa BWANA, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’ 26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litokee sawasawa.

27 “Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! 28 Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, Ee BWANA Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. 29 Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. 30 Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe.

31 “Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, 32 basi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie asiye na hatia kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kutokuwa na hatia kwake.

33 “Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, 34 basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.

35 “Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka katika dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, 36 basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.

37 “Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wo wote, maafa ya namna yo yote au ugonjwa wo wote unaoweza kuwajia, 38 wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akijua juu ya taabu ya moyo wake mwenyewe, akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili: 39 basi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), 40 ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.

41 “Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako, 42 kwa maana watu watasikia juu ya Jina lako kuu na juu ya mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, wakati atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili, 43 basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lo lote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli na wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.

44 “Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, po pote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa BWANA kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 45 basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao.

46 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu ye yote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao nakuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu; 47 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda kwa uovu’; 48 kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako; 49 basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na ukawatetee haki yao. 50 Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma; 51 kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka kwenye lile tanuru lakuyeyushia chuma.

52 “Macho yako na yafumbuke juu ya ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wo wote wanapokulilia. 53 Kwa maana uliwachagua wao kutoka mataifa yote ya ulimwengu kuwa urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Mose wakati wewe, Ee BWANA Mwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.”54 Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwa BWANA, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya BWANA, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni. 55 Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa akisema:

56 “Ahimidiwe BWANA, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose. 57 BWANA Mungu wetu na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa. 58 Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kuzishika amri na maagizo na masharti aliyowapa baba zetu. 59 Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za BWANA, yawe karibu na BWANA Mungu wetu mchana na usiku, ili kwamba atetee shauri la mtumishi wake na la watu wake Israeli kulingana na hitaji lao la kila siku, 60 ili kwamba mataifa yote ya dunia wajue kwamba BWANA ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine. 61 Lakini ni lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa BWANA Mungu wetu, kuishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.”

Kuwekwa Wakfu Hekalu

62 Kisha mfalme na Israeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za BWANA. 63 Solomoni akatoa dhabihu sadaka za amani kwa BWANA: ng'ombe 22,000, kondoo pamoja na mbuzi 120,000. Hivyo mfalme pamoja na Waisraeli wote wakaliweka wakfu Hekalu la BWANA.

64 Siku iyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya kati ya ua ulioko mbele ya Hekalu la BWANA na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani.

65 Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Israeli wote pamoja naye: walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka ingilio la Hamathi hadi Korongo la Misri. Wakiadhimisha mbele za BWANA Mungu wetu kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani, jumla siku kumi na nne. 66 Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani, wakiwa na mashangilio na furaha rohoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo BWANA ametenda kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.

Copyright information for Neno