1 Peter 3

Mafundisho Kwa Wake Na Waume

1Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama wako wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno, 2kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu. 3Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi. 4Badala yake kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa ndani, kwa uzuri usioharibika, wa roho ya upole na utulivu, ambako ni kwa thamani sana machoni pa Mungu. 5Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao, 6kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema na bila kuogopa jambo lo lote.

7Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha thamani cha uzima, ili kusiwepo na cho chote cha kuzuia maombi yenu.

Kuteseka Kwa Kutenda Mema

8Hatimaye, ninyi nyote iweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, wasikitivu na wanyenyekevu. 9Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka. 10Kwa maana, “Ye yote apendaye uzima
na kuona siku njema,
basi auzuie ulimi wake usinene mabaya
na midomo yake isiseme hila.
11Mtu huyo lazima aache ubaya, akatende mema;
atafute amani na kuifuatilia sana.
12Kwa maana macho ya Bwana
huwaelekea wenye haki,
na masikio yake
husikiliza maombi yao,
bali uso wa Bwana ni dhidi yao
watendao maovu.”


Kuvumilia Mateso

13Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye bidii katika kutenda mema? 14Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao wala msiwe na wasiwasi.” 15Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu ye yote atakayewauliza kuhusu tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima, 16mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo, waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

17Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu. 18Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho, 19ambayo kwa hiyo alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni. 20Roho hizo ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Noa, wakati wa kujenga safina, ambako watu wachache tu, yaani, watu wanane waliokolewa wasiangamie kwa gharika. 21Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia, si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo, 22ambaye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu: pamoja na malaika, mamlaka na nguvu zote vikiwa vimetiishwa chini yake.

Copyright information for Neno