1 Peter 4

Kuishi Kwa Ajili Ya Mungu

Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. Matokeo yake, maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani, haishi tena kwa kufuata tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu. Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo watu wasiomjua Mungu hupenda kutenda, wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya na ibada za sanamu ambazo ni chukizo. Wao huona kuwa ni ajabu ninyi kutokujiingiza tena pamoja nao katika huo wingi wa ufisadi, nao huwatukana ninyi. Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili kwamba wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi sawasawa na Mungu aishivyo.

Kuja Kwa Kristo Kumekaribia

Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo iweni na akili pia mwe na kiasi mkikesha katika kuomba. Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi. Iweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manung'uniko. 10 Kila mmoja na atumie kipawa cho chote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu. 11 Ye yote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Ye yote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile apewazo na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

Kuteseka Kwa Kuwa Mkristo

12 Wapenzi, msione ajabu katika yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata. 13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili kwamba mpate kufurahi zaidi na kushangilia wakati utukufu wake utakapofunuliwa. 14 Kama mkilaumiwa kwa ajili ya Jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yenu. 15 Lakini asiwepo mtu ye yote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni mwuaji, au mwivi, au mhalifu au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine, ili kuwagombanisha. 16 Lakini kama mtu ye yote akiteseka kwa kuwa ni mkristo, asihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali amtukuze Mungu kwa sababu ameitwa kwa jina hilo. 17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianza kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje? 18 Basi, “Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka,
itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu
na mwenye dhambi?”19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa sawasawa na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.

Copyright information for Neno