1 Peter 5

Kulichunga Kundi La Mungu

1Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa, 2lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe, si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika. 3Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali iweni vielelezo kwa hilo kundi. 4Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika.

5Vivyo hivyo ninyi mlio vijana hamna budi kuwatii wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu katika kuhudumiana, kila mtu na mwenzake, kwa kuwa, “Mungu huwapinga wenye kiburi
bali huwapa wanyenyekevu neema.”6Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake. 7Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote kwa maana hujishughulisha sana na mambo yenu.

8Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi, kama simba angurumaye huzungukazunguka akitafuta mtu ili apate kummeza. 9Mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso yayo hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

10Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawatengeneza upya, atawasaidia, atawatia nguvu na kuwathibitisha. 11Uweza una yeye milele na milele. Amen.

Salamu Za Mwisho

12Kwa msaada wa Silvano
5:12 Yaani Sila
, yeye ambaye ninamhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.

13Kanisa lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu. 14Salimianeni kwa busu la upendo.

Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo. Amen.

Copyright information for Neno