1 Peter 1

Salamu

1Petro, mtume wa Yesu Kristo:

Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia.
2Ninawaandikia ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utii na kunyunyizwa damu ya Yesu Kristo:

Neema iwe nanyi na amani iongezwe kwenu.

Tumaini Lenye Uzima

3Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu, 4ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu, 5ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. 6Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi. 7Haya yamewajia ili kwamba uhalisi wa imani yenu (yenye thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto) ionekane kuwa katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 8Ambaye, ingawa hamjamwona, mnampenda, tena ingawa sasa hamumwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka. 9Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

10Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, 11wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. 12Mitume walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali walihudumu kwa ajili yenu katika mambo hayo ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo ambayo hata malaika wanatamani kuyafahamu.

Mwito Wa Kuishi Maisha Matakatifu

13Kwa hiyo, vifungeni viuno vya nia zenu, mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa, Yesu Kristo atakapodhihirishwa. 14Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya za kwanza za wakati wa ujinga. 15Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote, 16kwa maana imeandikwa: “Mtakuwa watakatifu, kwa kuwa Mimi ni mtakatifu.”

17Nanyi kama mnamwita Baba yeye ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni. 18Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo, yaani, kwa fedha na dhahabu, 19bali kwa damu ya thamani ya Kristo, kama ile ya Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa. 20Yeye aliwekewa hayo kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu, 21ambaye kwa yeye mmemwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

22Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli kwa njia ya Roho kwa kuwapenda ndugu zenu kwa upendo wa kweli, pendaneni kwa dhati kutoka moyoni. 23Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu hata milele. 24Maana, “Watu wote ni kama majani,
na utukufu wao ni kama ua la shambani;
majani hunyauka na ua lake hupukutika,
25lakini neno la Mungu ladumu milele.”Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.

Copyright information for Neno