1 Peter 2

Jiwe Lililo Hai Na Watu Waliochaguliwa

1Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna. 2Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine cho chote, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu, 3ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.

4Mwendeeni yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake. 5Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa kuwa nyumba ya Roho, mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. 6Kwa maana Andiko lasema: “Tazama, naweka katika Sayuni,
Jiwe Kuu la pembeni,
teule lenye thamani,
na kila amwaminiye
hataaibika.”7Kwenu ninyi mnaoamini, yeye ni wa thamani. Lakini kwao wasioamini, “Jiwe lile walilolikataa waashi
limekuwa Jiwe Kuu la pembeni,”8tena, “Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae,
mwamba wa kuwafanya waanguke.”Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno: kama walivyowekewa tangu zamani.

9Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu la Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. 10Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamkupata rehema, lakini sasa mmepata rehema. 11Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. 12Mwe na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasema kuwa ninyi ni watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema wamtukuze Mungu siku atakapokuja kuhukumu.

Kuwatii Wenye Mamlaka

13Tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu kwa ajili ya Bwana: Mfalme akiwa ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi, 14pamoja na maafisa aliowaweka. Kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa na kuwasifu wale watendao mema. 15Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu. 16Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu. 17Mheshimuni kila mtu. Wapendeni jamaa ya waaminio. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme.

18Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali. 19Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya kumkumbuka Mungu. 20Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la sifa mbele za Mungu.

Mfano Wa Mateso Ya Kristo

21Kwa kuwa ninyi mliitwa kwa ajili ya hayo, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake. 22“Yeye hakutenda dhambi,
wala udanganyifu haukuonekana
kinywani mwake.”23Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano, alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki. 24Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili kwamba tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa. 25Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.

Copyright information for Neno