1 Samuel 12

Hotuba Ya Samweli Ya Kuaga

1Samweli akawaambia Israeli wote, “Nimesikiliza kila kitu mlichoniambia nami nimewawekea mfalme juu yenu. 2Sasa mnaye mfalme kama kiongozi wenu. Lakini kwa habari yangu mimi ni mzee na nina mvi, nao wanangu wapo hapa pamoja nanyi. Nimekuwa kiongozi wenu tangu ujana wangu mpaka siku hii ya leo. 3Mimi ninasimama hapa. Shuhudieni juu yangu mbele za BWANA na mpakwa mafuta wake. Nimechukua maksai wa nani? Nimechukua punda wa nani? Ni nani nimepata kumdanganya? Ni nani nimepata kumwonea? Ni kutoka kwenye mkono wa nani nimepokea rushwa ili kunifanya nifumbe macho yangu? Kama nimefanya cho chote katika hivi, mimi nitawarudishia.”

4Wakajibu, “Hujatudanganya wala kutuonea. Hujapokea cho chote kutoka kwenye mkono wa mtu awaye yote.”

5Samweli akawaambia, “BWANA ni shahidi juu yenu, pia mpakwa mafuta wake ni shahidi siku hii ya leo, kwamba hamkukuta cho chote mkononi mwangu.”

Wakasema, “Yeye ni shahidi.”

6Kisha Samweli akawaambia watu, “BWANA ndiye aliyemchagua Mose na Aroni na kuwaleta baba zenu akiwapandisha kutoka Misri. 7Sasa basi, simameni hapa, kwa sababu ninakwenda kukabiliana nanyi kwa ushahidi mbele za BWANA kwa matendo yote ya haki yaliyofanywa na BWANA kwenu na kwa baba zenu.

8“Baada ya Yakobo kuingia Misri, walimlilia BWANA kwa ajili ya msaada, naye BWANA akawatuma Mose na Aroni, ambao waliwatoa baba zenu kutoka Misri na kuwakalisha mahali hapa.

9“Lakini wakamsahau BWANA Mungu wao, hivyo Mungu akawauza katika mkono wa Sisera, jemadari wa jeshi la Hazori na katika mikono ya Wafilisti na mfalme wa Moabu, ambaye alipigana dhidi yao. 10Wakamlilia BWANA na kusema, ‘Tumetenda dhambi; tumemwacha BWANA na kutumikia Mabaali na Maashtorethi. Lakini sasa tuokoe kutoka katika mikono ya adui zetu, nasi tutakutumikia.’ 11Ndipo BWANA akawatuma Yerub-Baali
12.11 Yerub-Baali pia aliitwa Gideoni
, Baraka, Yeftha na Samweli, naye akawaokoa kutoka katika mikono ya adui zenu kila upande, ili ninyi mpate kukaa salama.

12“Lakini mlipomwona yule Nahashi mfalme wa Waamoni anakuja dhidi yenu, mliniambia, ‘Hapana, tunataka mfalme atutawale,’ hata ingawa BWANA Mungu wenu alikuwa mfalme wenu. 13Sasa huyu hapa ndiye mfalme mliyemchagua, yule mliyeomba; tazameni, BWANA amemweka mfalme juu yenu. 14Kama mkimcha BWANA na kumtumikia na kumtii nanyi msipoasi dhidi ya amri zake, ninyi pamoja na mfalme anayetawala juu yenu mkimfuata BWANA, Mungu wenu, mambo yatakuwa mema kwenu! 15Lakini kama hamkumtii BWANA, nanyi kama mkiasi dhidi ya amri zake, mkono wake utakuwa dhidi yenu, kama ulivyokuwa dhidi ya baba zenu.

16“Sasa basi, simameni kimya mkaone jambo hili kubwa ambalo BWANA anakwenda kulifanya mbele ya macho yenu! 17Je, sasa si mavuno ya ngano? Nitamwomba BWANA ili alete ngurumo na mvua. Nanyi mtatambua jambo hili lilivyo baya mlilolifanya mbele za macho ya BWANA mlipoomba mfalme.”

18Kisha Samweli akamwomba BWANA, na siku ile ile BWANA akatuma ngurumo na mvua. Hivyo watu wote wakamwogopa sana BWANA na Samweli.

19Watu wote wakamwambia Samweli, “Mwombe BWANA Mungu wako kwa ajili ya watumishi wako, ili tusije tukafa, kwa kuwa tumeongeza uovu juu ya dhambi zetu nyingine kwa kuomba mfalme.”

20Samweli akajibu, “Msiogope, mmefanya uovu huu wote; hata hivyo msimwache BWANA, bali mtumikieni BWANA kwa moyo wenu wote. 21Msigeukie sanamu zisizofaa. Haziwezi kuwatendea jema, wala haziwezi kuwaokoa kwa sababu hazina maana. 22Kwa ajili ya jina lake kuu BWANA hatawakataa watu wake, kwa sababu ilimpendeza BWANA kuwafanya kuwa wake mwenyewe. 23Kwa habari yangu, iwe mbali nami kutenda dhambi dhidi ya BWANA kwa kushindwa kuwaombea. Mimi nitawafundisha njia iliyo njema na ya kunyooka. 24Lakini hakikisheni mnamcha BWANA na kumtumikia kwa uaminifu kwa moyo wenu wote, tafakarini ni mambo gani makubwa aliyotenda kwa ajili yenu. 25Hata hivyo mkiendelea kufanya uovu, ninyi na mfalme wenu mtafutiliwa mbali!”

Copyright information for Neno