1 Samuel 14

1Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake.

2Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu kama 600, 3miongoni mwao alikuwepo Ahiya, ambaye alikuwa amevaa kisibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo. Hakuna ye yote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka.

4Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwepo na jabali, jabali moja lilikuwa linaitwa Bosesi na jingine Sene. 5Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba.

6Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda BWANA atatenda kwa ajili yetu. Hakuna cho chote kitakachoweza kumzuia BWANA kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”

7Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyonayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.”

8Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. 9Kama wakituambia, ‘Subirini hapo mpaka tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. 10Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba BWANA amewatia mikononi mwetu.”

11Basi wote wawili wakajionyesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” 12Watu wa kwenye doria wakawapigia kelele Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njoni pandeni kwetu nasi tutawakomesha.”

Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu, BWANA amewatia mikononi mwa Israeli.”

13Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. 14Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka.

Israeli Wawafukuza Wafilisti

15Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo nchi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.

16Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote. 17Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka katikati yetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo.

18Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.) 19Wakati Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.”

20Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake. 21Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na ambao walikuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. 22Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii. 23Hivyo BWANA akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.

Yonathani Ala Asali

24Basi watu wa Israeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu ye yote ambaye atakula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu ye yote katika jeshi aliyeonja chakula.

25Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwepo na asali ardhini. 26Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu ye yote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo. 27Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakawa maangavu. 28Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu ye yote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.”

29Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi nilivyopata nguvu mpya nilipoonja asali hii kidogo. 30Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangalikula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?”

31Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi mpaka Aiyaloni, walikuwa wamechoka. 32Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ng'ombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. 33Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya BWANA kwa kula nyama yenye damu ndani yake.”

Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.”
34Kisha akasema, “Nendeni miongoni mwa watu na waambieni, ‘Kila mmoja wenu aniletee ng'ombe wake na kondoo, wachinjeni hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya BWANA, kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ”

Hivyo kila mmoja akaleta ng'ombe wake jioni ile na kumchinja hapo.
35Ndipo Sauli akamjengea BWANA madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu.

36Sauli akasema, “Tutelemke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara mpaka mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.”

Wakajibu, “Fanya lo lote lile uonalo jema zaidi kwako.”

Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.”

37Basi Sauli akamwuliza Mungu, akisema, “Je, nitelemke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile.

38Kwa hiyo Sauli akasema, “Njoni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo. 39Kwa hakika kama BWANA aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa juu ya mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu ye yote aliyesema neno.

40Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.”

Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.”

41Kisha Sauli akamwomba BWANA, Mungu wa Israeli, akisema, “Nipe jibu lililo sawa.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama. 42Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani.

43Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.”

Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu, Je, sasa ni lazima nife?”

44Sauli akasema, “Mungu na anishughulikie kwa ukali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.”

45Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta wokovu huu mkubwa Israeli? Hasha! Hakika kama BWANA aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa.

46Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao.

47Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Po pote alipogeukia, aliwashinda. 48Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka katika mikono ya wale ambao walikuwa wamewateka nyara.

Jamaa Ya Sauli

49Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa aliitwa Merabu, na mdogo aliitwa Mikali. 50Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti wa Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli. 51Babaye Sauli yaani, Kishi na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli.

52Siku zote za kutawala kwa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wo wote Sauli alipomwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.

Copyright information for Neno