1 Samuel 16

Samweli Anamtia Daudi Mafuta

BWANA akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli mpaka lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.”

Lakini Samweli akasema, “Nitakwendaje? Sauli atasikia juu ya jambo hili na ataniua.”

BWANA akamwambia, “Chukua mtamba wa ng'ombe na useme, ‘Nimekuja kumtolea BWANA dhabihu.’
Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakalofanya. Utamtia mafuta kwa ajili yangu yule nitakayekuonyesha.”

Samweli akafanya kile BWANA alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?”

Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu.

Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa BWANA anasimama hapa mbele za BWANA.”

Lakini BWANA akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. BWANA hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini BWANA hutazama moyoni.”

Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu BWANA hakumchagua.” Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu BWANA hakumchagua.” 10 Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “BWANA hajawachagua hawa.” 11 Hivyo akamwuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?”

Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.”

Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi mpaka afike.”

12 Basi akatuma aitwe naye akaletwa. Alikuwa mwekundu, mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza.

Ndipo BWANA akasema, “Inuka na umtie mafuta, huyu ndiye.”

13 Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumtia mafuta mbele ya ndugu zake, kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa BWANA akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama.

Daudi Katika Utumishi Kwa Sauli

14 Basi Roho wa BWANA alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na BWANA ili imtese.

15 Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Angalia, roho mbaya imeachiwa nafasi na BWANA nayo inakutesa. 16 Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walioko hapa kutafuta mtu ambaye anaweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.”

17 Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.”

18 Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa wa vita. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. BWANA yu pamoja naye.”

19 Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” 20 Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe.

21 Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha zake. 22 Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.”

23 Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.

Copyright information for Neno