1 Samuel 27

Daudi Miongoni Mwa Wafilisti

Daudi akasema moyoni mwake, “Katika mojawapo ya siku hizi nitaangamizwa kwa mkono wa Sauli. Jambo lililo bora ni kutorokea kwenye nchi ya Wafilisti. Hivyo Sauli atakata tamaa ya kunisaka po pote katika Israeli, nami nitakuwa nimeponyoka mkononi mwake.”

Hivyo Daudi akaondoka na hao watu mia sita waliokuwa pamoja naye na kwenda kwa Akishi mwana wa Maoki mfalme wa Gathi. Daudi na watu wake wakakaa huko Gathi pamoja na Akishi. Kila mtu alikuwa pamoja na jamaa yake, naye Daudi pamoja na wakeze wawili, yaani Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, mjane wa Nabali. Sauli alipokuwa ameambiwa kwamba Daudi alikuwa amekimbilia Gathi, hakuendelea kumsaka tena.

Ndipo Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali machoni pako, unipe sehemu katika mojawapo ya miji katika nchi nikae huko, kwa nini mtumwa wako akae pamoja nawe katika mji huu wa kifalme?”

Hivyo siku hiyo Akishi akampa Daudi mji wa Siklagi, nao Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda tangu wakati huo. Daudi akaishi katika nchi ya Wafilisti muda wa mwaka mmoja na miezi minne.

Basi Daudi na watu wake wakapanda na kuwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki. (Tangu zamani haya mataifa yalikuwa yameishi kwenye eneo lililotanda kuanzia Telemu katika njia itelemkayo Shuri hadi kufikia nchi ya Misri.) Kila mara Daudi aliposhambulia eneo, hakubakiza hai mwanaume wala mwanamke, lakini alichukua kondoo na ng'ombe, punda na ngamia, na nguo. Kisha akarudi kwa Akishi.

10 Akishi alipomwuliza, “Je leo umeshambulia wapi?” Daudi humjibu, “Dhidi ya Negebu ya Yuda” au wakati mwingine husema, “Dhidi ya Negebu ya Yerameeli” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni”. 11 Daudi hakumwacha hai mwanaume au mwanamke ili apate kuletwa Gathi, kwa maana Daudi aliwaza, “Wanaweza kujulisha habari zetu na kusema, ‘Hivi ndivyo alivyofanya Daudi.’ ” Hii ndiyo iliyokuwa desturi yake wakati wote alipoishi katika nchi ya Wafilisti. 12 Akishi akamsadiki Daudi na kuwaza moyoni mwake, akasema, “Daudi amekuwa kitu cha kuchukiza kabisa kwa watu wake, Waisraeli, hivi kwamba atakuwa mtumishi wangu milele.”

Copyright information for Neno