1 Samuel 30

Daudi Aangamiza Waamaleki

Daudi na watu wake wakafika Siklagi siku ya tatu. Basi Waamaleki walikuwa wamevamia Negebu na Siklagi. Wakawa wameshambulia mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto, nao wakawa wamewachukua mateka wanawake pamoja na wote waliokuwamo humo, vijana na wazee. Hawakuua ye yote, bali waliwachukua wakaenda zao.

Daudi na watu wake walipofika Siklagi, wakakuta mji umeangamizwa kwa moto na wake zao pamoja na wana wao na binti zao wamechukuliwa mateka. Hivyo Daudi na watu wake wakapiga yowe mpaka wakaishiwa na nguvu za kulia. Wake wawili wa Daudi walikuwa wametekwa, yaani Ahinoamu wa Yezreeli na Abigaili, mjane wa Nabali wa Karmeli. Daudi alihuzunika sana kwa sababu watu walikuwa wakisemezana juu ya kumpiga kwa mawe. Kila mmoja alikuwa na uchungu rohoni kwa sababu ya wanawe na binti zake. Lakini Daudi akajitia nguvu katika BWANA, Mungu wake.

Kisha Daudi akamwambia kuhani Abiathari, mwana wa Ahimeleki, “Niletee kile kisibau.” Abiathari akamletea, naye Daudi akamwuliza BWANA, “Je, nifuatie kundi hili la wavamizi? Je, nitawapata?”

BWANA akajibu, “Wafuatie. Hakika utawapata na utafanikiwa kuwaokoa.”

Daudi pamoja na watu wake 600 wakafika kwenye Bonde la Besori, mahali ambapo wengine waliachwa nyuma, 10 kwa kuwa watu 200 walikuwa wamechoka sana kuweza kuvuka hilo bonde. Lakini Daudi pamoja na watu 400 wakaendelea kufuatia.

11 Wakamkuta Mmisri katika shamba fulani, nao wakamleta kwa Daudi. Wakampa huyo Mmisri maji ya kunywa na chakula, 12 kipande cha andazi la tini na andazi la zabibu zilizokaushwa. Akala naye akapata nguvu, kwa kuwa hakuwa amekula chakula cho chote wala kunywa maji kwa siku tatu mchana na usiku.

13 Daudi akamwuliza, “Wewe ni wa nani, na umetoka wapi?”

Akajibu, “Mimi ni Mmisri, mtumwa wa Mwamaleki. Bwana wangu alinitelekeza nilipougua siku tatu zilizopita.
14 Tulivamia Negebu ya Wakerethi, na nchi ya Yuda, na Negebu ya Kalebu. Nasi tulichoma moto Siklagi.”

15 Daudi akamwuliza, “Je, unaweza kuniongoza kufikia kundi hili la uvamizi?”

Akajibu, “Niapie mbele ya Mungu kwamba hutaniua wala kunikabidhi mikononi mwa bwana wangu, nami nitakupeleka hadi waliko.”

16 Akamwongoza Daudi mpaka mahali walipokuwa, nao walikuwa wametawanyika eneo lote, wakila, wakinywa na wakifanya karamu kwa sababu ya nyara nyingi walizochukua kutoka katika nchi ya Wafilisti na kutoka Yuda. 17 Daudi akapigana nao kuanzia machweo ya jua hadi kesho yake jioni, na hakuna ye yote miongoni mwao aliyetoroka, isipokuwa vijana wanaume 400 waliopanda ngamia na kutoroka. 18 Daudi akarudisha kila kitu Waamaleki walichokuwa wamechukua, pamoja na wake zake wawili. 19 Hakuna cho chote kilichopotea kijana au mzee, mvulana au msichana, nyara au kitu kingine cho chote walichokuwa wamechukua. Daudi akarudisha kila kitu. 20 Akachukua makundi yote ya kondoo, mbuzi na ng'ombe, nao watu wake wakawaswaga wanyama hao mbele ya wanyama wengine wa kufugwa, wakisema, “Hizi ni nyara za Daudi.”

21 Kisha Daudi akafika kwa wale watu 200 waliokuwa wamechoka sana kumfuata na ambao waliachwa nyuma kwenye Bonde la Besori. Wakatoka kwenda kumlaki Daudi na wale watu aliokuwa nao. Daudi na watu wake walipowakaribia, akawasalimu. 22 Lakini watu wote waovu na wakorofi miongoni mwa wafuasi wa Daudi wakasema, “Kwa sababu hawakwenda pamoja nasi, hatutagawana nao nyara tulizorudisha. Lakini, kila mtu aweza kuchukua mkewe na watoto wake na kuondoka.”

23 Daudi akajibu, “La hasha, ndugu zangu, kamwe hamwezi kufanya hivyo kwa kile ambacho BWANA ametupatia. Yeye ametulinda na kuweka mikononi mwetu majeshi yale yaliyokuja kupigana dhidi yetu. 24 Ni nani atasikiliza yale mnayosema? Fungu la mtu aliyekaa na vyombo litakuwa sawa na la yule aliyekwenda vitani. Wote watashiriki sawa.” 25 Daudi akafanya hili liwe amri na agizo kwa Israeli kutoka siku ile hata leo.

26 Daudi alipofika Siklagi, akatuma baadhi ya nyara kwa wazee wa Yuda, waliokuwa rafiki zake, akasema, “Tazama, hapa kuna zawadi kwa ajili yenu kutoka katika nyara za adui za BWANA.”

27 Akazituma kwa wale waliokuwa Betheli, Ramoth-Negebu na Yatiri; 28 kwa wale walioko Aroeri, Sifmothi, Eshtemoa 29 na Rakali; kwa wale waliokuwa katika miji ya Wayerameeli na ya Wakeni; 30 na kwa wale walioko Horma, Bori-Ashani, Athaki, 31 na kwa wakazi wa Hebroni; na kwa wale waliokuwa mahali pengine pote ambako Daudi na watu wake walitembelea.

Copyright information for Neno