1 Samuel 2

Maombi Ya Hana

1Kisha Hana akaomba na kusema:

“Moyo wangu wamshangilia BWANA,
katika BWANA pembe yangu imeinuliwa juu.
Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu,
kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
2“Hakuna ye yote aliye mtakatifu kama BWANA,
hakuna mwingine zaidi yako;
hakuna Mwamba kama Mungu wetu.
3“Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo
wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi,
kwa kuwa BWANA ndiye Mungu ajuaye,
na kwa yeye matendo hupimwa.
4“Pinde za mashujaa zimevunjika,
lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.
5Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe
ili kupata chakula,
lakini wale waliokuwa na njaa
hawana njaa tena.
Mwanamke yule aliyekuwa tasa
amezaa watoto saba,
lakini yule ambaye alikuwa na wana wengi
amedhoofika.
6“BWANA huua na huleta uhai,
hushusha chini mpaka kaburini
2.6 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol
na kufufua.
7BWANA humfanya mtu maskini naye hutajirisha,
hushusha na hukweza.
8Humwinua maskini kutoka mavumbini
na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu;
huwaketisha pamoja na wakuu
na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima.
“Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya BWANA;
juu yake ameuweka ulimwengu.
9Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake,
lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza.
“Si kwa nguvu mtu hushinda;
10wale wampingao BWANA
wataharibiwa kabisa.
Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni;
BWANA ataihukumu miisho ya dunia.
“Atampa nguvu mfalme wake,
na kuitukuza pembe
ya mpakwa mafuta
2.10 Mpakwa mafuta maana yake ni Masiya
wake.”11Kisha Elikana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za BWANA chini ya kuhani Eli.

Wana Waovu Wa Eli

12Wana wa Eli walikuwa watu wabaya kabisa, hawakumheshimu BWANA. 13Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara ye yote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake. 14Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angalijichukulia mwenyewe cho chote ambacho uma ungelikileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo. 15Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na kusema kwa mtu ambaye alikuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.”

16Kama mtu akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, kisha ndipo uchukue cho chote unachotaka,” mtumishi angalijibu, “Hapana, nipe sasa, kama huwezi nitaichukua kwa nguvu.”

17Hii Dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya BWANA kwa dharau.

18Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za BWANA, kijana akivaa kisibau cha kitani. 19Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumchukulia wakati alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka. 20Eli alikuwa akiwabariki Elikana na mkewe, akisema, “BWANA na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa BWANA.” Kisha wakawa wanakwenda nyumbani. 21BWANA akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za BWANA.

22Basi Eli, ambaye alikuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania. 23Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote juu ya haya matendo yenu maovu. 24Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ambayo ninasikia ikienea miongoni mwa watu wa BWANA. 25Kama mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu BWANA alitaka kuwaua.

26Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza BWANA na wanadamu.

Unabii Dhidi Ya Nyumba Ya Eli

27Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walipokuwa huko Misri chini ya Farao? 28Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kisibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli. 29Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka zile nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula zile sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?

30“Kwa hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa BWANA anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa. 31Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika mbari yenu atakayeishi kuuona uzee 32nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watafanyiwa mema, katika mbari yenu kamwe hapatakuwepo mtu atakayeishi hadi kuwa mzee. 33Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi.

34“ ‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja. 35Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaifanya nyumba yake kuwa imara, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima. 36Kisha kila mmoja aliyeachwa katika mbari yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.” ’ ”

Copyright information for Neno