1 Samuel 3

BWANA Amwita Samweli

1Kijana Samweli alihudumu mbele za BWANA chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwepo na maono mengi.

2Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida. 3Taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala Hekaluni
3.3 Hekaluni maana yake ndani ya Maskani ya BWANA
mwa BWANA, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwako.
4Kisha BWANA akamwita Samweli.

Samweli akajibu, “Mimi hapa.”
5Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala.

6BWANA akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita”

Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.”

7Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua BWANA. Neno la BWANA lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

8BWANA akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Ndipo Eli akatambua kuwa BWANA alikuwa akimwita kijana.
9Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale, na kama akikuita, sema, ‘Nena BWANA, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake.

10BWANA akaja akasimama hapo, akiita kama mara zile nyingine, “Samweli! Samweli!”

Kisha Samweli akasema, “Nena BWANA, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”

11Naye BWANA akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. 12Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo mpaka mwisho. 13Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. 14Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”

15Samweli akalala mpaka asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya BWANA. Aliogopa kumwambia Eli yale maono, 16lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.”

Samweli akamjibu, “Mimi hapa.”

17Eli akamwuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. BWANA na ashughulike nawe, tena kwa ukali, kama utanificha cho chote alichokuambia.” 18Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu, bila kumficha cho chote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni BWANA; na afanye lile lililo jema machoni pake!”

19BWANA alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha hata moja ya maneno yake lianguke chini. 20Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa BWANA. 21BWANA akaendelea kutokea huko Shilo, na huko kujidhihirisha kwa Samweli kwa njia ya neno lake.

Copyright information for Neno