1 Samuel 31

Sauli Ajiua

1Basi Wafilisti wakapigana dhidi ya Israeli. Waisraeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, na wengi wakauawa kwenye Mlima wa Gilboa. 2Wafilisti wakawasonga Sauli na wanawe kwa nguvu, na kuwaua wanawe Yonathani, Abinadabu na Malki-Shua. 3Mapigano yakawa makali sana kumzunguka Sauli, nao wapiga upinde wakampata na kumjeruhi vibaya.

4Sauli akamwambia mchukua silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa jamaa wasiotahiriwa watakuja kunichoma na kunitendea vibaya.”

Lakini mchukua silaha wake aliogopa na hakuweza kufanya hivyo, basi Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia.
5Mchukua silaha wake alipoona Sauli amekufa, naye pia akaangukia upanga wake akafa pamoja naye. 6Basi Sauli, wanawe watatu, mchukua silaha wake na watu wake wote wakafa pamoja siku ile ile.

7Waisraeli waliokuwa kandokando ya bonde na wale waliokuwa ng'ambo ya Yordani walipoona kuwa jeshi la Waisraeli limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, wakaacha miji yao na kukimbia. Nao Wafilisti wakaja na kumiliki humo.

8Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, wakamkuta Sauli na wanawe watatu wameanguka kwenye Mlima Gilboa. 9Wakamkata Sauli kichwa na kumvua silaha zake, nao wakatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari katika hekalu la sanamu zao na miongoni mwa watu wao. 10Wakaweka silaha zake katika hekalu la Maashtorethi, na kukifunga kiwiliwili chake katika ukuta wa Beth-Shani.

11Watu wa Yabeshi-Gileadi waliposikia kile Wafilisti walichomfanyia Sauli, 12mashujaa wao wote wakaenda usiku hadi Beth-Shani. Wakauchukua mwili wa Sauli na miili ya wanawe kutoka kwenye ukuta wa Beth-Shani na kurudi hadi Yabeshi, mahali ambapo waliiteketeza kwa moto. 13Kisha wakachukua mifupa yao na kuizika chini ya mti wa mkwaju huko Yabeshi, nao wakafunga siku saba.

Copyright information for Neno