1 Samuel 4

1Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote.

Wafilisti Wateka Sanduku La Mungu

Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki.
2Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao 4,000 kwenye uwanja wa vita. 3Wakati Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa nini BWANA ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tulete Sanduku la Agano la BWANA kutoka Shilo, ili kwamba lipate kwenda pamoja nasi na kutuokoa kutoka mkono wa adui zetu.”

4Hivyo wakatumwa watu kwenda Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la BWANA Mwenye Nguvu Zote, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao wale wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, walikuwako huko pamoja na S anduku la Agano la Mungu.

5Wakati Sanduku la Agano la BWANA lilipokuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. 6Wafilisti waliposikia makelele wakauliza, “Ni nini makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?”

Walipofahamu kuwa Sanduku la BWANA limekuja kambini,
7Wafilisti wakaogopa wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo. 8Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. 9Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Iweni wanaume, mpigane!”

10Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia hemani mwake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari 30,000 waendao kwa miguu. 11Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.

Kifo Cha Eli

12Siku ile ile mtu mmoja wa kabila la Benyamini akakimbia kutoka kwenye uwanja wa vita na kwenda Shilo, nguo zake zikiwa zimeraruka na akiwa na mavumbi kichwani mwake. 13Alipofika, Eli alikuwa ameketi juu ya kiti chake kando ya barabara akiangalia, kwa sababu moyo wake ulikuwa na hofu kwa ajili ya Sanduku la Mungu. Mtu yule alipoingia mjini na kueleza ni nini kilichokuwa kimetokea, mji wote ukalia.

14Eli akasikia kelele za kilio, naye akauliza, “Ni nini maana ya makelele haya?”

Yule mtu akafanya haraka kwenda kwa Eli,
15wakati huu Eli alikuwa na miaka tisini na minane nayo macho yake yalikuwa yamepofuka na hakuweza kuona. 16Akamwambia Eli, “Mimi nimetoka vitani sasa hivi, nimekimbia kutoka huko leo hii.”

Eli akamwuliza, “Je, mwanangu, ni nini kimetokea huko?”

17Yule mtu aliyeleta habari akajibu, “Israeli amekimbia mbele ya Wafilisti, nalo jeshi limepata hasara kubwa. Pia wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa, na Sanduku la Mungu limetekwa.”

18Mara alipotaja Sanduku la Mungu, Eli alianguka kutoka kwenye kiti chake kwa nyuma kando ya lango. Shingo yake ikavunjika naye akafa, kwa kuwa alikuwa mzee tena mzito. Alikuwa amewaongoza Israeli kwa miaka arobaini.

19Mkwewe, mke wa Finehasi, alikuwa mja mzito na karibu wakati wa kujifungua. Aliposikia habari kwamba Sanduku la Mungu limetekwa na yakuwa baba mkwe wake na mumewe wamekufa, akapata utungu naye akajifungua lakini akazidiwa na utungu. 20Alipokuwa akifa, wanawake waliokuwa wanamhudumia wakamwambia, “Usikate tamaa, umemzaa mwana.” Lakini hakujibu wala kuweka maanani.

21Alimwita yule mtoto Ikabodi
4.21 Ikabodi maana yake Utukufu wa BWANA umeondoka
, akisema, “Utukufu umeondoka katika Israeli,” kwa sababu ya kutekwa kwa Sanduku la Mungu na vifo vya baba mkwe na muwewe.
22Akasema, “Utukufu umeondoka katika Israeli, kwa kuwa Sanduku la Mungu limetekwa.”

Copyright information for Neno