1 Timothy 2

Maagizo Kuhusu Kuabudu

Awali ya yote, nasihi, kwanza kabisa, naagiza kwamba dua, sala, maombezi na shukrani zifanyike kwa ajili ya watu wote: kwa ajili ya wafalme na wale wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi kwa amani na utulivu, katika uchaji wote wa Mungu na utakatifu. Jambo hili ni jema tena linapendeza machoni pa Mungu Mwokozi wetu anayetaka watu wote waokolewe na wafikie kuijua kweli. Kwa maana kuna Mungu mmoja na mpatanishi mmoja kati ya Mungu na wanadamu, yaani, mwanadamu Kristo Yesu, aliyejitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wanadamu wote: jambo hili lilishuhudiwa kwa wakati wake. Nami kwa kusudi hili nimewekwa niwe mhubiri na mtume (nasema kweli katika Kristo wala sisemi uongo), mwalimu wa watu Mataifa katika imani na kweli.

Nataka kila mahali wanaume wasali wakiinua mikono mitakatifu pasipo hasira wala kugombana.

Vivyo hivyo nataka wanawake wajipambe kwa adabu na kwa heshima katika mavazi yanayostahili, si kwa kusuka nywele, kuvalia dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa, 10 bali kwa matendo mazuri kama iwapasavyo wanawake wanaokiri kuwa wanamcha Mungu.

11 Mwanamke na ajifunze kwa utulivu na kwa utii wote. 12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha au kuwa na mamlaka juu ya mwanaume. Mwanamke inampasa kukaa kimya. 13 Kwa maana Adamu aliumbwa kwanza, kisha Eva. 14 Wala si Adamu aliyedanganywa, bali ni mwanamke aliyedanganywa akawa mkosaji. 15 Lakini mwanamke ataokolewa kwa kuzaa kwake kama wakiendelea kudumu katika imani, upendo na utakatifu, pamoja na kuwa na kiasi.

Copyright information for Neno