1 Timothy 3

Sifa Za Waangalizi

Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) Asiwe mtu aliyeongoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya Shetani. Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi.

Sifa Za Mashemasi

Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. 10 Ni lazima wapimwe kwanza, kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi.

11 Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasiozungumza maneno ya kuwadhuru wengine, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo.

12 Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. 13 Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu.

14 Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba, 15 kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli. 16 Bila shaka yo yote, siri ya utauwa ni kubwa: Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu,
akathibitishwa kuwa na haki katika Roho,
akaonekana na malaika,
akahubiriwa miongoni mwa mataifa,
akaaminiwa ulimwenguni,
akachukuliwa juu katika utukufu.


Copyright information for Neno