2 Chronicles 18

Mikaya Atoa Unabii Dhidi Ya Ahabu

Basi, Yehoshafati alikuwa na mali nyingi sana na heshima. Naye akafanya urafiki na Ahabu kwa mwanawe kumwoa binti wa Ahabu. Baada ya miaka kadhaa akashuka kumtembelea Ahabu huko Samaria. Ahabu akachinja ng'ombe na kondoo wengi kwa ajili yake na watu aliokuwa amefuatana nao. Kisha Ahabu akamshawishi Yehoshafati kukwea pamoja naye ili kuishambulia Ramoth-Gileadi. Ahabu mfalme wa Israeli akamwuliza Yehoshafati mfalme wa Yuda, “Je, utakwenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?”

Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako. Tutakuwa pamoja nawe vitani.”
Lakini Mfalme Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta shauri la BWANA.”

Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii wanaume wapatao 400, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?”

Wakajibu, “Naam, nenda kwa kuwa BWANA ataitiya Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”

Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa BWANA hapa ambaye tunaweza kumwuliza?”

Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia yeye twaweza kumwuliza shauri la BWANA, lakini namchukia kwa sababu huwa hatabiri jambo lo lote jema kunihusu mimi, lakini kila mara hunitabiria mabaya tu. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”

Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”

Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”

Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, pamoja na manabii wote wakiwa wakitabiri mbele yao. 10 Wakati huu Zedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma na akatangaza, “Hivi ndivyo BWANA asemavyo, ‘Kwa hizi pembe utawapiga na kuwarudisha Waaramu nyuma mpaka wameangamizwa.’ ”

11 Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa BWANA ataitia mkononi mwa mfalme.”

12 Mjumbe aliyekuwa amekwenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”

13 Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo, nitamwambia kile tu BWANA atakachoniambia.”

14 Alipofika, mfalme akamwuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?”

Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa BWANA atawatia mkononi mwa mfalme.”

15 Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu cho chote ila kweli tu kwa jina la BWANA?”

16 Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye BWANA akasema, ‘Watu hawa hawana bwana. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”

17 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lo lote jema kunihusu bali mabaya tu?”

18 Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la BWANA: Nilimwona BWANA ameketi juu ya kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama kumzunguka kulia kwake na kushoto kwake. 19 Naye BWANA akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’

“Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
20 Mwishoni, roho akajitokeza, akasimama mbele za BWANA na kusema, ‘Nitamshawishi.’

“BWANA akauliza, ‘Kwa njia gani?’

21 “Akasema, ‘Nitakwenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’

“BWANA akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’

22 “Kwa hiyo sasa BWANA ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. BWANA ameamuru maafa kwa ajili yako.”

23 Kisha Zedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa BWANA alipita njia gani, alipotoka kwangu ili kusema nawe?”

24 Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapokwenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”

25 Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni na mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme. 26 Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe cho chote ila mkate na maji mpaka nitakaporudi salama.’ ”

27 Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi BWANA hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”

Ahabu Anauawa Huko Ramoth-Gileadi

28 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi. 29 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.

30 Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na mtu ye yote, mdogo wala mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.” 31 Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele, 32 wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli nao wakaacha kumfuatilia.

33 Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma, mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.” 34 Vita vikaendelea mchana kutwa naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa.

Copyright information for Neno