2 Chronicles 22

Ahazia Mfalme Wa Yuda

1Watu wa Yerusalemu wakamfanya Ahazia, mdogo wa wote wa wana wa Yerohamu, kuwa mfalme mahali pa baba yake, kwa sababu washambuliaji wa ghafula waliokuwa wameingia kambini pamoja na Waarabu, walikuwa wamewaua wana wakubwa wote wa Yehoramu. Kwa hiyo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akaanza kutawala.

2Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipokuwa mfalme, naye akatawala huko Yerusalemu kwa mwaka mmoja. Mama yake aliitwa Athalia mjukuu wa kike wa Omri.

3Ahazia naye akaziendea njia za nyumba ya Ahabu kwa sababu mama yake alikuwa mshauri wake katika kutenda maovu. 4Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA kama walivyokuwa wamefanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa baada ya kufa kwa baba yake nyumba ya Ahabu ndio waliokuwa washauri wake, kwa uangamivu wake. 5Pia akafuata shauri lao alipokwenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli kupigana na Hazaeli mfalme wa Aramu huko Ramoth-Gileadi. Waaramu wakamjeruhi Yoramu, 6hivyo akarudi Yezreeli ili apate kuuguza majeraha aliyokuwa ameyapata huko Ramoth
22.6 Yaani Rama kwa Kiebrania
, kwenye vita vyake na Hazaeli mfalme wa Aramu.

Ndipo Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda, akashuka kwenda Yezreeli kumtazama Yoramu mwana wa Ahabu kwa sababu alikuwa amejeruhiwa.

7Mungu alikuwa ameamuru kwamba kuanguka kwa Ahazia kungetokea atakapokwenda kumwona Yoramu. Ahazia alipowasili, wakatoka pamoja na Yoramu ili kwenda kukutana na Yehu mwana wa Nimshi, ambaye BWANA alikuwa amemtia mafuta kuangamiza nyumba ya Ahabu. 8Yehu alipokuwa anatekeleza hukumu juu ya nyumba ya Ahabu, akawakuta wakuu wa Yuda na wana wa jamaa ya Ahazia waliokuwa wanamhudumia Ahazia, naye akawaua. 9Ndipo akaenda kumsaka Ahazia, nao watu wake wakamkamata alipokuwa amejificha huko Samaria. Akaletwa kwa Yehu, naye Yehu akamwua. Wakamzika kwani walisema, “Alikuwa mwana wa Yehoshafati, ambaye alimtafuta BWANA kwa moyo wake wote.” Hivyo hapakuwa na mtu mwenye uwezo katika nyumba ya Ahazia aliyeweza kushika ufalme.

Athalia na Yoashi

10Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akaondoka akawaua wazao wote wa kifalme wa nyumba ya Yuda. 11Lakini Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu akamchukua Yoashi mwana wa Ahazia na kumwiba miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa wanakaribia kuuawa. Akamweka yeye pamoja na yaya wake kwenye chumba cha kulala. Kwa kuwa Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu, mkewe Kuhani Yehoyada, alikuwa dada yake Ahazia, akamficha mtoto ili Athalia asimwue. 12Akawa pamoja nao akiwa amefichwa katika Hekalu la Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alipokuwa anatawala nchi.

Copyright information for Neno