2 Chronicles 28

Ahazi Mfalme Wa Yuda

Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala. Akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa BWANA. Akaziendea njia za wafalme wa Israeli na pia akasubu sanamu kwa ajili ya kuabudu Mabaali. Akatoa sadaka za kuteketezwa katika Bonde la Hinomu na kuwatoa wanawe kafara kwa kuwateketeza kwa moto, akifuata njia za machukizo za yale mataifa BWANA aliyoyafukuza humo mbele ya Waisraeli. Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu, juu ya vilima na chini ya kila mti wenye majani mabichi uliotanda.

Kwa hiyo BWANA Mungu wake akamtia mikononi mwa mfalme wa Aramu. Waaramu wakamshinda, wakachukua watu wake wengi mateka na kuwaleta mpaka Dameski.

Tena alitiwa mikononi mwa mfalme wa Israeli, ambaye aliwaua watu wake wengi.
Kwa siku moja Peka mwana wa Remalia aliwaua askari 120,000 katika Yuda, kwa kuwa Yuda walikuwa wamemwacha BWANA, Mungu wa baba zao. Zikri, askari shujaa Mwefraimu, akamwua Maaseya mwana wa mfalme, Azrikamu mkuu wa jumba la kifalme na Elikana aliyekuwa wa pili kwa mfalme. Waisraeli wakawachukuwa mateka kutoka ndugu zao, watu wapatao 200,000 hawa wakiwa ni wanawake, watoto wa kiume na wa kike. Wakachukua pia kiasi kikubwa cha nyara, ambazo walirudi nazo Samaria.

Lakini kulikuwako huko nabii wa BWANA aliyeitwa Odedi, akaondoka ili kukutana na jeshi liliporejea Samaria. Akawaambia, “Kwa kuwa BWANA, Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, aliwatia mikononi mwenu. Lakini mmewachinja kwa hasira ambayo imefika hadi mbinguni. 10 Nanyi sasa mnakusudia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Lakini ninyi je, hamna pia hatia ya dhambi mliyotenda dhidi ya BWANA Mungu wenu? 11 Basi nisikilizeni! Mkawarudishe mateka mliowachukua kutoka kwa ndugu zenu, kwa kuwa hasira kali ya BWANA iko juu yenu.”

12 Ndipo baadhi ya viongozi katika Efraimu, yaani, Azaria mwana wa Yehohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, wakakubaliana na huyo nabii, hivyo wakawapinga wale waliokuwa wanawasili kutoka vitani. 13 Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele za BWANA. Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali ya BWANA iko juu ya Israeli.”

14 Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote. 15 Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukuwa wale mateka na kutoka katika zile nyara, wakachukua mavazi wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao mpaka Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.

Waashuru Wakataa Kusaidia Yuda

16 Wakati ule, Mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada. 17 Waedomu walikuwa wamekuja tena na kuwashambulia Yuda na kuchukua mateka. 18 Pia Wafilisti walikuwa wameshambulia miji iliyokuwa chini ya vilima na katika miji ya Negebu ya Yuda. Nao wakawa wametwaa Beth-Shemeshi, Aiyaloni, Gederothi, Soko pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake, Gimzo pia pamoja na vijiji vyake na kuishi humo. 19 BWANA aliishusha Yuda kwa sababu ya Ahazi mfalme wa Israeli, kwa kuwa alikuwa ameongeza uovu katika Yuda na kumkosea BWANA mno. 20 Hivyo Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru akaja kumtesa badala ya kumsaidia. 21 Ahazi akachukua baadhi ya vitu kutoka katika Hekalu la BWANA, jumba la kifalme na kutoka kwa wakuu wake na kumpa mfalme wa Ashuru kama ushuru, lakini hilo halikumsaidia.

22 Katika wakati wake wa mateso Mfalme Ahazi akazidi kukosa uaminifu kwa BWANA. 23 Akatoa kafara kwa miungu ya Dameski, ambao walikuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie na mimi.” Lakini haya ndiyo yaliyokuwa maangamizi yake na Israeli wote.

24 Ahazi akakusanya pamoja vyombo vya nyumba ya Mungu na kuvivunja vipande vipande. Akafunga milango ya Hekalu la BWANA na kusimamisha madhabahu katika kila njia panda ya barabara za Yerusalemu. 25 Katika kila mji wa Yuda akajenga mahali pa juu pa kuabudia miungu ili kutolea miungu mingine kafara za kuteketezwa na kuchochea hasira ya BWANA, Mungu wa baba zake.

26 Matukio mengine ya utawala wake na njia zake nyingine zote, tangu mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli. 27 Ahazi akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Yerusalemu, lakini hawakumleta kwenye makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Copyright information for Neno