2 Chronicles 33

Manase Mfalme Wa Yuda

1Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano. 2Akafanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, akafanya machukizo kama walivyofanya mataifa BWANA aliyoyafukuza mbele ya Waisraeli. 3Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo Hezekia baba yake, alikuwa amepabomoa, pia akasimamisha madhabahu za Mabaali na nguzo za Maashera. Akalisujudia jeshi lote la vitu vya angani na kuliabudu. 4Akajenga madhabahu za Baali katika Hekalu la BWANA ambamo BWANA alikuwa amesema, “Jina langu litakaa Yerusalemu milele.” 5Katika nyua zote za Hekalu la BWANA akajengea madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la vitu vya angani. 6Akawatoa wanawe kuwa kafara kwa kuwapitisha katika moto katika Bonde la Hinomu, akafanya ulozi, uaguzi na uchawi, akataka ushauri kwa wenye pepo wa utambuzi na wenye kuwasiliana na mizimu. Akafanya maovu mengi machoni pa BWANA, akaichochea hasira yake.

7Akachukua ile sanamu aliyoichonga akaiweka katika Hekalu la BWANA ambalo Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Solomoni, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu niliouchagua kutoka kabila zote za Israeli, nitaliweka Jina langu milele. 8Sitaifanya miguu ya Waisraeli iondoke tena katika nchi niliyowapa baba zenu, kama watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru kuhusu sheria zote, maagizo na amri zilizotolewa kwa mkono wa Mose.” 9Lakini Manase akawaongoza Yuda na watu wa Yerusalemu katika upotovu, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kupita mataifa ambayo BWANA aliwaangamiza mbele ya Waisraeli.

10BWANA akasema na Manase pamoja na watu wake, lakini hawakumjali. 11Hivyo BWANA akaleta juu yao majemadari wa jeshi la mfalme wa Ashuru, ambao walimchukua Manase kwenda kifungoni, wakaweka ndoana katika pua yake, wakamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli. 12Katika dhiki yake akamsihi BWANA Mungu wake na kujinyenyekeza sana mbele za Mungu wa baba zake. 13Naye alipomwomba, BWANA akaguswa na kule kusihi kwake na akasikiliza kilio chake, kwa hiyo akamrudisha Yerusalemu na kwenye ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kwamba BWANA ndiye Mungu.

14Baadaye akajenga ukuta wa nje wa Mji wa Daudi, magharibi mwa chemchemi ya Gihoni katika bonde, hadi kufikia ingilio la Lango la Samaki na akakizunguka kilima cha Ofeli, pia akaufanya kuwa mrefu zaidi. Akawaweka majemadari katika miji yote ya Yuda iliyokuwa imejengewa ngome.

15Akaondolea mbali miungu ya kigeni na kuondoa sanamu kutoka katika Hekalu la BWANA pamoja na madhabahu zote alizozijenga katika kile kilima kilichojengwa Hekalu na katika Yerusalemu, akazitupa nje ya mji. 16Kisha akarudisha madhabahu ya BWANA na kutolea juu yake dhabihu za sadaka za amani pamoja na sadaka za shukrani, naye akawaamuru Yuda wamtumikie BWANA, Mungu wa Israeli. 17Lakini hata hivyo watu wakaendelea kutoa dhabihu mahali pa juu pa kuabudia miungu, lakini wakimtolea BWANA Mungu wao peke yake.

18Matukio mengine ya utawala wa Manase, maombi yake kwa Mungu wake na maneno aliyoambiwa na waonaji walionena naye kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli, yameandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Israeli. 19Maombi yake, pamoja na jinsi Mungu alivyoguswa na kusihi kwake, pia dhambi zake zote na kukosa kwake uaminifu pamoja na sehemu alizojenga mahali pa juu pa kuabudia miungu, kule kusimamisha nguzo za Ashera na sanamu kabla ya kujinyenyekeza kwake, yote yameandikwa katika kumbukumbu za waonaji. 20Manase akalala pamoja na baba zake akazikwa katika jumba lake la kifalme. Naye Amoni mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Amoni Mfalme Wa Yuda

21Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili, alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. 22Akafanya maovu machoni pa BWANA kama alivyokuwa amefanya Manase baba yake. Amoni akaabudu na kutoa dhabihu kwa sanamu zote alizokuwa ametengeneza Manase. 23Lakini tofauti na Manase baba yake, hakujinyenyekeza mbele za BWANA, badala yake Amoni aliongeza makosa zaidi na zaidi.

24Maafisa wa Amoni wakafanya shauri pamoja wakamwua katika jumba lake la kifalme. 25Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamefanya hila dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme badala yake.

Copyright information for Neno