2 Chronicles 9

Malkia Wa Sheba Amtembelea Solomoni

Malkia wa Sheba aliposikia habari za umaarufu wa Solomoni na uhusiano wake na jina la BWANA, huyo malkia akaja kumjaribu kwa maswali magumu. Alipofika Yerusalemu akiwa na msafara mkubwa sana, pamoja na ngamia waliobeba vikolezi, kiasi kikubwa cha dhahabu na vito vya thamani, alikuja kwa Solomoni na kuzungumza naye kuhusu yote ambayo alikuwa nayo moyoni mwake. Solomoni akamjibu maswali yake yote, wala hakukuwa na jambo lo lote lililokuwa gumu kwa mfalme asiweze kumwelezea. Malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Solomoni na jumba la kifalme alilokuwa amejenga, chakula kilichokuwa mezani pake, jinsi maafisa wake walivyokaa, wahudumu katika majoho yao, wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa Solomoni alizotoa katika Hekalu la BWANA alipatwa na mshangao.

Akamwambia mfalme, “Taarifa niliyosikia kwenye nchi yangu mwenyewe kuhusu mafanikio na hekima yako ni kweli. Lakini sikuamini mambo haya mpaka nilipokuja na kuona kwa macho yangu mwenyewe. Naam, sikuambiwa hata nusu yake; katika hekima na mali umezidi sana kuliko ile taarifa niliyoisikia. Heri watu wako! Heri hawa maafisa wako wasimamao mbele yako daima na kusikia hekima yako! Ahimidiwe BWANA Mungu wako, ambaye amependezwa sana nawe na kukuweka juu ya kiti chake cha ufalme kutawala kwa niaba ya BWANA Mungu wako. Kwa sababu ya upendo wa Mungu wako kwa Israeli na shauku yake ya kuwadhibitisha milele, amekufanya wewe mfalme juu yao, ili kudumisha haki na uadilifu.”

Naye akampa mfalme talanta 120
9.9 Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 4.5
za dhahabu, kiasi kikubwa cha vikolezi na mawe ya thamani. Haikuwahi kamwe kuletwa vikolezi vizuri kama vile Malkia wa Sheba alivyompa Mfalme Solomoni.

10 (Watumishi wa Hiramu na wa Solomoni wakaleta dhahabu kutoka Ofiri, tena wakaleta shehena kubwa ya miti ya msandali na mawe ya thamani. 11 Mfalme akatumia hiyo miti ya msandali kuwa ngazi kwa ajili ya Hekalu la BWANA na kwa jumba la kifalme, pia kwa kutengeneza vinubi na zeze kwa ajili ya waimbaji. Kiasi hicho kingi cha miti ya msandali hakikuwahi kuingizwa nchini tangu siku ile.)

12 Mfalme Solomoni akampa Malkia wa Sheba kila kitu alichohitaji na kukiomba, zaidi ya vile alivyokuwa amemletea mfalme. Kisha malkia akaondoka akarudi kwenye nchi yake mwenyewe pamoja na wafuasi wake.

Fahari Ya Solomoni

13 Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666
9.13 Talanta 666 za dhahabu ni sawa na tani 25
,
14 mbali na mapato mengine kutoka kwa wafanyibiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Solomoni dhahabu na fedha.

15 Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa ya dhahabu yenye uzito wa shekeli 600
9.15 Shekeli 600 za dhahabu ni sawa na kilo 3.5
.
16 Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa ya uzito wa mane tatu
9.16 Mane tatu za dhahabu ni sawa na kilo 1.7
za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.

17 Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi. 18 Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pakuwekea miguu vyote vya dhahabu. Upande wa kuume na wa kushoto wa hicho kiti palikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, pakiwa na sanamu ya simba iliyosimama kila upande. 19 Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, wawili kwenye kila ngazi, yaani, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wo wote. 20 Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Solomoni. 21 Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara
9:21 Au: meli nyingi za kwenda Tarshishi (ona pia 1 Fal 10:22; 22:48; 2 Nya 20:36; Isa 2:16; 60:9)
baharini zilizokuwa zikiandamana na meli za Hiramu. Mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wadogo na wakubwa.

22 Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia. 23 Dunia yote ikatafuta kukutana na Solomoni kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameweka katika moyo wake. 24 Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.

25 Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 kwa ajili ya farasi na magari ya vita, farasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita na katika Yerusalemu pamoja naye. 26 Solomoni akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto Eufrati mpaka kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri. 27 Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu na mierezi kuwa mingi kama miti ya mikuyu iliyoko chini ya vilima. 28 Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka nchi nyingine zote.

Kifo Cha Solomoni

29 Kwa habari ya matukio mengine ya utawala wa Solomoni, kuanzia mwanzo hadi mwisho, je, hayakuandikwa katika kumbukumbu za nabii Nathani, katika unabii wa Ahiya Mshiloni na katika maono ya Ido mwonaji dhidi ya Yeroboamu mwana wa Nebati? 30 Solomoni akatawala huko Yerusalemu juu ya Israeli yote kwa miaka arobaini. 31 Kisha Solomoni akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Copyright information for Neno