2 Chronicles 6

Kuweka Hekalu Wakfu

1Kisha Solomoni akasema, “BWANA alisema ya kwamba angelikaa katika wingu jeusi. 2Nimejenga Hekalu zuri kwa ajili yako, mahali pako pa kukaa milele.”

3Wakati kusanyiko lote la Israeli likiwa limesimama huko, Mfalme Solomoni akageuka na kuwabariki. 4Kisha akasema:

“Ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza lile alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa maana alisema,
5‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lo lote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo kwa ajili ya Jina langu, wala sikumchagua mtu ye yote kuwa kiongozi wa watu wangu Israeli. 6Lakini sasa nimeuchagua Yerusalemu ili Jina langu lipate kuwemo humo, nami nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’

7“Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. 8Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. 9Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni nyama yako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’

10“BWANA ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile BWANA alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wa Israeli. 11Nimeliweka humo Sanduku la Agano, ambalo ndani yake ndimo liliko lile Agano la BWANA alilofanya na watu wa Israeli.”

Maombi Ya Solomoni Ya Kuweka Wakfu

12Kisha Solomoni akasimama mbele ya madhabahu ya BWANA machoni pa kusanyiko lote la Israeli, naye akakunjua mikono yake. 13Basi alikuwa ametengeneza jukwaa la shaba, urefu wake dhiraa tano, na upana wake dhiraa tano na kimo chake dhiraa tatu, naye akaliweka katikati ya ukumbi wa nje. Akapanda juu ya hilo jukwaa kisha akapiga magoti mbele ya kushanyiko lote la Israeli, akanyosha mikono yake kwelekea mbinguni. 14Akasema:

“Ee BWANA, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe mbinguni juu wala duniani chini, wewe unayetunza Agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote.
15Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umelitimiza, kama ilivyo leo.

16“Sasa BWANA, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, kama wanao wakiangalia yote wayafanyayo kuenenda mbele zangu kama vile ulivyofanya.’ 17Sasa, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, acha neno lako lile ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie sawasawa.

18“Lakini kweli, je, Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! 19Hata hivyo sikiliza dua ya mtumishi wako na maombi yake kwa huruma, Ee BWANA Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambayo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. 20Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwako humo,’ ili kwamba upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. 21Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia kutoka mbinguni, mahali pa makao yako na usikiapo, samehe.

22“Mtu anapomkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, 23basi, sikia kutoka mbinguni na ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie asiye na hatia kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kutokuwa na hatia kwake.

24“Wakati watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, watakapokugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, 25basi usikie kutoka mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.

26“Wakati mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka katika dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, 27basi usikie kutoka mbinguni na usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.

28“Wakati njaa au tauni vikija juu ya nchi, au koga au kawa, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wo wote, maafa ya namna yo yote au ugonjwa wo wote unaoweza kuwajia, 29wakati dua au maombi yatakapofanywa na mmojawapo wa watu wako Israeli, kila mmoja akijua juu ya taabu ya moyo wake mwenyewe, akainyosha mikono yake kuelekea Hekalu hili, 30basi usikie kutoka mbinguni, katika makao yako. Usamehe na utende, umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), 31ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.

32“Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako kuu na mkono wako wenye nguvu ulionyoshwa, atakapokuja kuomba akikabili Hekalu hili, 33basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lo lote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.

34“Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, po pote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa BWANA kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 35basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao.

36“Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu ye yote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwatia mikononi mwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu 37na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowachukua mateka na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda kwa uovu’; 38kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 39basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na ukatetee haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako.

40“Sasa, Mungu wangu, macho yako na yafumbuke na masikio yako yasikie maombi yaombwayo mahali hapa. 41

“Sasa inuka, Ee BWANA Mungu,
na uje mahali pako pa kupumzika,
wewe na Sanduku la nguvu zako.
Makuhani wako, Ee BWANA Mungu,
na wavikwe wokovu,
watakatifu wako na wafurahi
katika wema wako.
42Ee BWANA Mungu, usimkatae
mpakwa mafuta wako.
Kumbuka upendo mkuu uliomwahidia
Daudi mtumishi wako.”


Copyright information for Neno