2 YOHANA

2 Yohana

Utangulizi

Waraka wa pili wa Yohana umeandikwa kwa Bibi mteule na watoto wake. Unaweza kuwa unamhusu mtu binafsi na jamaa yake, au kuna uwezekano kabisa kwamba unalihusu kanisa. Msisitizo umewekwa katika umuhimu wa imani kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu katika umbo la mwanadamu. Waumini wanaosoma inawapasa kudumu katika pendo la Mungu na kukataa mafundisho mapotovu ya imani.

Yohana pia aliandika kuwaonya ili waweze kutambua walimu wa uongo wanaosafiri huku na huko, wasije wakawaunga mkono na kuwasaidia. Yaani mtu ye yote asije akachangia kwenye kueneza mafundisho ya uongo badala ya yale ya kweli.Wazo Kuu

Mtume Yohana anaagiza watu kuenenda katika kweli na kumtii Mungu, wakijihadhari na udanganyifu ili wapate kumpenda Mungu na kupendana wao kwa wao.Mwandishi

Mtume Yohana.Kusudi

Kuhimiza mwenendo wa muumini, na maonyo kuhusu wadanganyifu na mbinu zao.Mambo Muhimu

Pendo la kweli ni kuwajali wengine.Tunatamani kupendwa na kuwapenda wengine, lakini tunaona mifano michache sana ya uhalisi katika jambo hili. Dunia imejaa ubinafsi, uchoyo na kujipenda yenyewe.Mahali

Efeso.Tarehe

Kama mwaka wa 90 B.K.Wahusika Wakuu

Yohana, bibi mteule na watoto wake.Mgawanyo

  • • Salamu (1:1-3)
  • • Ushauri na maonyo (1:4-11)
  • • Hitimisho (1:12-13).

2 John

Salamu

1Mzee:

Kwa bibi mteule na watoto wake, niwapendao katika kweli, wala si mimi tu, bali na wale wote waijuayo kweli:
2kwa sababu ya ile kweli ikaayo ndani yetu na ambayo itaendelea kukaa nasi milele:

3Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwanawe Baba, itakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

Kweli Na Upendo

4Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza. 5Sasa, bibi mpendwa, nakuomba, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Sisi na tupendane kila mmoja na mwenzake. 6Hili ndilo pendo, kwamba tuenende sawasawa na amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.

7Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametokea ulimwenguni. Mtu wa namna hiyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo. 8Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu. 9Mtu ye yote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Ye yote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia. 10Msimpokee mtu ye yote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu. 11Ye yote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.

Salamu Za Mwisho

12Ingawa ninayo mengi ya kuwaandikia, lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kwenu na kuongea nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.13Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu. Amen.

Copyright information for Neno