2 Kings 11

Athalia Na Yoashi

1Wakati Athalia mamaye Ahazia alipoona kwamba mwanawe amekufa, akainuka na kuiangamiza jamaa yote ya kifalme. 2Lakini Yehosheba, binti wa Mfalme Yehoramu ambaye ni dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa kifalme, ambao walikuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa. 3Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake kwenye Hekalu la BWANA kwa miaka sita wakati Athalia alipokuwa akitawala nchi.

4Katika mwaka wa saba Yehoyada kuhani akaamuru waletwe wakuu wa vikundi vya mamia wa Wakari
11.4 Yaani Wakerethi (ona 1 Sam 30:14; Ezek 25:16; Sef 2:5, 6)
na walinzi, nao wakaletwa kwake kwenye Hekalu la BWANA. Akafanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la BWANA. Ndipo akawaonyesha mwana wa mfalme.
5Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaokwenda zamu siku ya Sabato, theluthi yenu itakuwa ikilinda jumba la kifalme, 6theluthi nyingine italinda Lango la Suri, na theluthi nyingine italinda lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu; 7nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme. 8Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi mwake. Ye yote anayesogelea safu yenu ya askari ni lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme po pote aendako.”

9Majemadari wa vikosi vya mamia wakafanya sawasawa kama alivyoagiza kuhani Yehoyada. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakienda zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa katika mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada. 10Ndipo akawapa wale majemadari mikuki na ngao zilizokuwa mali ya Mfalme Daudi na zile zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA. 11Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.

12Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano na kumtangaza kuwa mfalme. Wakamtia mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”

13Athalia aliposikia kelele iliyofanywa na walinzi pamoja na watu, akawaendea watu pale penye Hekalu la BWANA. 14Akaangalia na tazama alikuwako mfalme, akiwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa pembeni mwa mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wakifurahi na kupiga tarumbeta. Kisha Athalia akararua majoho yake na kupiga kelele, “Uhaini! Uhaini!”

15Kuhani Yehoyada akawaagiza majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa wasimamizi wa jeshi, “Mleteni huyo Athalia nje katikati ya safu, na mtieni upanga mtu ye yote atakayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la BWANA.” 16Basi wakamkamata Athalia na alipofika mahali ambapo farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamwulia hapo.

17Ndipo Yehoyada akafanya Agano kati ya BWANA na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa BWANA. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu. 18Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunja madhabahu zote na sanamu vipande vipande na kumwua Matani kuhani wa Baali mbele ya hiyo madhabahu.

Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la BWANA.
19Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamshusha mfalme kutoka katika Hekalu la BWANA na kwenda kwenye jumba la kifalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha enzi, 20nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga huko kwenye jumba la kifalme.

21Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba wakati alipoanza kutawala.

Copyright information for Neno