2 Kings 17

Hoshea, Mfalme Wa Mwisho Katika Israeli

Katika mwaka wa kumi na mbili wa kutawala kwake Ahazi mfalme wa Yuda, Hoshea mwana wa Ela akawa mfalme wa Israeli katika Samaria, akatawala kwa miaka tisa. Akafanya maovu machoni pa BWANA, lakini si kama wafalme wengine wa Israeli waliomtangulia.

Mfalme Shalmanesa wa Ashuru akainuka dhidi ya Mfalme Hoshea, ambaye hapo mbeleni alikuwa mtumwa wake na kumlipa ushuru. Lakini mfalme wa Ashuru akagundua kuwa Hoshea alikuwa msaliti, kwa kuwa alikuwa ametuma wajumbe kwa So mfalme wa Misri, naye hakuendelea kulipa ushuru kwa mfalme wa Ashuru tena kama alivyokuwa anafanya kila mwaka. Kwa hiyo Shalmanesa akamkamata na kumtia gerezani. Mfalme wa Ashuru akaishambulia nchi yote, akapigana dhidi ya Samaria na kuizunguka kwa majeshi miaka mitatu. Katika mwaka wa tisa wa Hoshea, mfalme wa Ashuru akaiteka Samaria na kuwahamishia Waisraeli huko Ashuru. Akawaweka huko Hala, Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi.

Israeli Inakwenda Uhamishoni Kwa Sababu Ya Dhambi

Yote haya yalitokea kwa sababu Waisraeli walikuwa wametenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wao, ambaye alikuwa amewapandisha kutoka Misri akiwatoa chini ya utawala wa nguvu wa Farao mfalme wa Misri. Waliabudu miungu mingine na kufuata desturi za mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao, pamoja na desturi ambazo wafalme wa Israeli walizileta. Waisraeli wakafanya vitu kwa siri dhidi ya BWANA Mungu wao, ambavyo havikuwa sawa. Kuanzia kwenye mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye maboma walijijengea wenyewe mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji yao yote. 10 Wakaweka mawe ya kuabudiwa na nguzo za Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda. 11 Wakafukiza uvumba kila mahali palipoinuka, kama walivyofanya yale mataifa ambayo BWANA alikuwa ameyafukuza mbele yao. Wakafanya mambo maovu ambayo yalimghadhibisha BWANA. 12 Wakaabudu sanamu, ingawa BWANA alikuwa amesema, “Msifanye mambo haya.” 13 BWANA akawaonya Israeli na Yuda kupitia kwa manabii na waonaji wake wote: “Acheni njia zenu mbaya. Zishikeni amri na maagizo yangu, sawasawa na sheria yangu yote niliyowaagiza baba zenu kuitii ambayo niliileta kwenu kupitia kwa watumishi wangu manabii.”

14 Lakini hawakusikiliza, walikuwa na shingo ngumu kama baba zao, ambao hawakumtegemea BWANA Mungu wao. 15 Walizikataa amri zake na Agano alilokuwa amelifanya na baba zao na maonyo aliyokuwa amewapa. Wakafuata sanamu zisizofaa, nao wenyewe wakawa hawafai. Wakayaigiza mataifa yaliyowazunguka, ingawa BWANA alikuwa amewaonya akiwaambia, “Msifanye kama wanavyofanya,” nao wakafanya mambo ambayo BWANA alikuwa amewakataza wasifanye.

16 Wakayaacha maagizo yote ya BWANA Mungu wao na kujitengenezea sanamu mbili walizozisubu katika sura ya ndama na nguzo ya Ashera. Wakasujudia mianga yote ya angani, wakamtumikia Baali. 17 Wakawatoa kafara wana wao na mabinti zao katika moto. Wakafanya uaguzi na uchawi, nao wakajiuza wenyewe katika kutenda uovu machoni pa BWANA, wakamghadhibisha.

18 Basi BWANA akawakasirikia sana Israeli na kuwaondoa kwenye uwepo wake. Ni kabila la Yuda tu ndilo lililobaki; 19 hata hivyo nao hawakuzishika amri za BWANA Mungu wao. Wakafuata desturi ambazo Israeli alikuwa amezileta. 20 Kwa hiyo BWANA aliwakataa watu wote wa Israeli; akawatesa na kuwaachia katika mikono ya wateka nyara hadi alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake.

21 Alipokwisha kuwatenga Israeli mbali na nyumba ya Daudi, wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme wao. Yeroboamu akawashawishi Israeli waache kumfuata BWANA na akawasababisha kutenda dhambi kuu. 22 Nao Israeli wakadumu katika dhambi zote za Yeroboamu mwana wa Nebati, hawakuziacha 23 hadi BWANA alipowaondoa kutoka kwenye uwepo wake, kama vile alivyokuwa ameonya kupitia watumishi wake wote manabii. Hivyo watu wa Israeli wakaondolewa kutoka katika nchi yao kwenda uhamishoni Ashuru, nao wako huko mpaka sasa.

Samaria Inakaliwa Tena

24 Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake. 25 Wakati walipoanza kuishi humo, hawakumwabudu BWANA, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu. 26 Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.”

27 Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.” 28 Basi mmoja wa makuhani ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli na kuwafundisha jinsi ya kumwabudu BWANA.

29 Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka mahali pa ibada za miungu ambapo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu. 30 Watu kutoka Babeli wakamtengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakamtengeneza Nergali na watu kutoka Hamathi wakamtengeneza Ashima; 31 Waavi wakamtengeneza Nibhazi na Tartaki, Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki miungu ya Sefarvaimu. 32 Walimwabudu BWANA, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu pa ibada za miungu. 33 Walimwabudu BWANA, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.

34 Mpaka leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu BWANA wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo BWANA aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli. 35 Wakati BWANA alipofanya Agano na Waisraeli aliwaamuru akisema: “Msiiabudu miungu mingine yo yote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu. 36 Bali imewapasa kumwabudu BWANA aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu na kwake yeye mtatoa dhabihu. 37 Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine. 38 Msisahau Agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine. 39 Bali, mtamwabudu BWANA Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”

40 Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali. 41 Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu BWANA, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Mpaka leo watoto wao na watoto wa watoto wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.

Copyright information for Neno