2 Kings 18

Hezekia Mfalme Wa Yuda

Katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake Hoshea mwana wa Ela mfalme wa Israeli, Hezekia mwana wa Ahazi mfalme wa Yuda alianza kutawala. Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala katika Yerusalemu kwa miaka ishirini na tisa. Jina la mama yake aliitwa Abiya binti Zekaria. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA, kama Daudi baba yake alivyofanya. Akapaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu, akazivunja sanamu, akakatakata nguzo za Ashera. Akavunja vipande vipande ile nyoka ya shaba Mose aliyotengeneza, kwa kuwa hadi siku hizo wana wa Israeli walikuwa wanaifukizia uvumba (nayo ilikuwa ikiitwa Nehushtani
18.4 Nehushtani maana yake Kipande cha shaba
).

Hezekia aliweka tumaini lake kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Hapakuwepo na mfalme mwingine wa kufanana naye miongoni mwa wafalme wa Yuda, kabla yake au baada yake. Alishikamana na BWANA kwa bidii wala hakuacha kumfuata; alishika amri ambazo BWANA alikuwa amempa Mose. Naye BWANA alikuwa pamoja naye, akafanikiwa katika kila alichokifanya. Aliasi dhidi ya mfalme wa Ashuru na wala hakumtumikia. Kuanzia mnara wa ulinzi hadi kwenye mji wenye ngome, aliwashinda Wafilisti, hadi kufikia Gaza na himaya yake yote.

Mwaka wa nne wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa saba wa Hoshea mwana wa Ela kutawala Israeli, Shalmanesa mfalme wa Ashuru alikwenda kuishambulia Samaria na kuuzunguka kwa majeshi. 10 Baada ya miaka mitatu Waashuru wakautwaa. Kwa hiyo Samaria ulitekwa katika mwaka wa sita wa utawala wa Mfalme Hezekia, ambao ulikuwa mwaka wa tisa wa kutawala kwake Hoshea mfalme wa Israeli. 11 Mfalme wa Ashuru akawahamishia Waisraeli huko Ashuru na akawaweka Hala, Gozani karibu na Mto Habori, na katika miji ya Wamedi. 12 Hili lilitokea kwa sababu walikuwa hawakumtii BWANA Mungu wao, lakini walikuwa wamevunja Agano lake, yale yote ambayo Mose mtumishi wa BWANA aliwaamuru. Hawakuzisikiliza amri wala kuzitimiza.

13 Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda iliyozungushiwa ngome na kuitwaa. 14 Basi Hezekia mfalme wa Yuda akamtumia ujumbe mfalme wa Ashuru huko Lakishi akisema: “Nimefanya makosa. Ondoka katika nchi yangu, nami nitakulipa cho chote unachokitaka kwangu.” Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia mfalme wa Yuda talanta 300
18.14 Talanta 300 za fedha ni sawa na tani 10
za fedha na talanta thelathini
18.14 Talanta 30 za dhahabu ni sawa na tani moja
za dhahabu.
15 Basi Hezekia akampa fedha yote iliyopatikana ndani ya Hekalu la BWANA na katika hazina ya jumba la kifalme.

16 Wakati huu Hezekia mfalme wa Yuda akabandua dhahabu yote iliyokuwa imefunika milango na miimo ya Hekalu la BWANA, akampa mfalme wa Ashuru.

Senakeribu Anaitishia Yerusalemu

17 Mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wake mkuu, na afisa wake mkuu, na jemadari wa jeshi lake pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi mpaka kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Wakaja mpaka Yerusalemu na kusimama kando ya mfereji unaopeleka maji katika Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi. 18 Wakaagiza mfalme aitwe; Eliyakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, na Shebna mwandishi, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wa kumbukumbu, nao wakawaendea.

19 Yule jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia:

“ ‘Hivi ndivyo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru asemavyo: Ni wapi unapoweka hilo tumaini lako?
20 Unasema unazo mbinu na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Ni nani unayemtegemea hata kuasi dhidi yangu? 21 Tazama, sasa unategemea Misri, ile fimbo ya mwanzi iliyopasuka, ambayo huuchoma mkono wa mtu na kumjeruhi kama akiuegemea. Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri kwa ye yote anayemtegemea. 22 Nawe kama ukiniambia, “Tunamtumaini BWANA Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu zake, akisema kwa Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu hii katika Yerusalemu”?

23 “ ‘Njoni sasa, mfanye majadiliano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapata wapanda farasi elfu mbili! 24 Wewe na hilo jeshi lako dogo utawezaje kumzuia hata afisa mmoja wa kundi dogo na dhaifu la jeshi la bwana wangu, ijapo unaitegemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi? 25 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza mahali hapa pasipo neno kutoka kwa BWANA? BWANA mwenyewe ndiye aliyeniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”26 Kisha Eliyakimu mwana wa Hilkia, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa Kiaramu, kwa kuwa tunakielewa vizuri. Usiseme nasi kwa Kiebrania wakati hao watu walio juu ya ukuta wanasikia.”

27 Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioko ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mikojo yao wenyewe?”

28 Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa Kiebrania: “Sikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru! 29 Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa mkononi mwangu. 30 Msimkubali Hezekia awashawishi kumtumaini BWANA kwa kuwaambia, ‘Hakika BWANA atatuokoa; mji huu hautaangukia mkononi mwa mfalme wa Ashuru.’

31 “Msimsikilize Hezekia. Hivi ndivyo asemavyo mfalme wa Ashuru: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwenye mzabibu wake mwenyewe na kwenye mtini wake na kunywa maji kutoka kwenye kisima chake mwenyewe, 32 mpaka nitakapokuja na kuwapeleka kwenye nchi iliyo kama hii ya kwenu, nchi yenye nafaka na divai mpya, nchi ya mikate na mashamba ya mizabibu, nchi ya mizeituni na asali. Chagueni uzima na sio mauti!

“Msimsikilize Hezekia, kwa kuwa anawapotosha wakati anaposema, ‘BWANA atatuokoa.’
33 Je, yuko mungu wa taifa lo lote aliyeiokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru? 34 Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, Hena na Iva? Je, imeweza kuiokoa Samaria kutoka mkononi mwangu? 35 Je, ni nani kati ya miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake kutoka kwangu? Itawezekanaje basi, BWANA aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”

36 Lakini wale watu wakakaa kimya hawakujibu lo lote, kwa sababu Mfalme Hezekia alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lo lote.”

37 Kisha Eliyakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna mwandishi na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wa kumbukumbu wakamwendea Mfalme Hezekia, wakiwa wamerarua nguo zao, wakamwambia yale waliyoambiwa na yule jemadari wa jeshi.

Copyright information for Neno