2 Kings 2

Eliya Achukuliwa Juu Mbinguni

1Wakati BWANA alipokuwa karibu kumchukua Eliya juu mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya na Elisha walikuwa njiani kutoka Gilgali. 2Eliya akamwambia Elisha, “Kaa hapa, BWANA amenituma Betheli.”

Lakini Elisha akasema, “Kwa hakika, kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo wakaenda Betheli pamoja.

3Wana wa manabii walikuwako huko Betheli wakamjia Elisha na kumwuliza, “Je, unajua ya kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?”

Elisha akawajibu, “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”

4Kisha Eliya akamwambia, “Baki hapa Elisha, BWANA amenituma Yeriko.”

Naye akajibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wakaenda Yeriko.

5Wana wa manabii waliokuwako huko Yeriko wakamwendea Elisha na kumwuliza, “Je, unajua ya kwamba BWANA atakuondolea bwana wako leo?”

Akawajibu “Ndiyo, najua, lakini msizungumze juu ya jambo hilo.”

6Kisha Eliya akamwambia, “Kaa hapa, BWANA amenituma kwenda Yordani.”

Naye akamjibu, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Hivyo wote wawili wakaendelea pamoja.

7Wana hamsini wa manabii wakaenda na kusimama kwa mbali, kuelekea mahali ambapo Eliya na Elisha walikuwa wamesimama katika Mto Yordani. 8Eliya akachukua vazi lake, akalisokota na kupiga nalo maji. Maji yakagawanyika upande wa kuume na upande wa kushoto, nao wawili wakavuka pakavu.

9Walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, “Niambie, nikufanyie nini kabla sijaondolewa kutoka kwako?”

Elisha akajibu, “Naomba nirithi sehemu maradufu ya roho yako.”

10Eliya akasema, “Umeomba jambo gumu, lakini kama utaniona wakati ninapoondolewa kutoka kwako litakuwa lako, la sivyo, haitakuwa hivyo.”

11Walipokuwa wakitembea pamoja na kuzungumza, ghafula gari la moto na farasi wa moto vilitokea na kuwatenganisha wao wawili, naye Eliya akapanda mbinguni katika upepo wa kisulisuli. 12Elisha aliona hili akapaza sauti, “Baba yangu! Baba yangu! Magari ya Israeli na wapanda farasi wake!” Naye Elisha hakumwona tena. Kisha akazishika nguo zake mwenyewe na kuzichana.

13Akaliokota lile vazi lililoanguka kutoka kwa Eliya, kisha akarudi na kusimama ukingoni mwa Yordani. 14Ndipo akalichukua lile vazi ambalo lilikuwa limeanguka kutoka kwa Eliya naye akayapiga nalo yale maji. Akauliza, “Yuko wapi sasa BWANA, Mungu wa Eliya?” Alipoyapiga maji, yakagawanyika kulia na kushoto, naye akavuka.

15Wale wana wa manabii kutoka Yeriko, waliokuwa wakitazama, wakasema, “Roho wa Eliya inamkalia Elisha.” Nao wakaenda kumlaki na kusujudu hadi nchi mbele yake. 16Wakasema, “Tazama, sisi watumishi wako tunao watu hamsini wenye uwezo. Waruhusu waende kumtafuta bwana wako. Labda Roho wa BWANA amemtwaa na kumweka katika mlima fulani au bonde fulani.”

Elisha akajibu, “Hapana, msiwatume.”

17Lakini wakasisitiza mpaka akaona aibu kuwakatalia. Hivyo akasema, “Watumeni.” Nao wakawatuma watu hamsini, wakamtafuta kwa siku tatu, lakini hawakumpata. 18Walipomrudia Elisha, ambaye alikuwa akingojea huko Yeriko, akawaambia, “Je, sikuwaambia msiende?”

Kuponywa Kwa Maji

19Watu wa mji wakamwambia Elisha, “Tazama, bwana wetu, mahali mji huu ulipojengwa ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo, lakini maji yake ni mabaya na nchi haizai.”

20Akasema, “Nileteeni bakuli mpya, wekeni chumvi ndani yake.” Kwa hiyo wakamletea.

21Kisha akatoka akaenda kwenye chemchemi na kuitupa ile chumvi ndani yake, akisema, “Hili ndilo asemalo BWANA: ‘Nimeyaponya maji haya. Kamwe hayatasababisha mauti tena wala kutozaa.’ ” 22Nayo yale maji yakaponywa mpaka leo, sawasawa na neno la Elisha alilokuwa amesema.

Elisha Anafanyiwa Mzaha

23Kutoka huko Elisha akakwea kwenda Betheli. Ikawa alipokuwa akitembea barabarani, baadhi ya vijana wakatoka mjini na kumfanyia mzaha. Wakisema, “Paa, wewe mwenye upaa! Paa, wewe mwenye upaa!” 24Akageuka, akawatazama na kuwalaani kwa Jina la BWANA. Kisha dubu wawili wa kike wakatokea mwituni na kuwararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao. 25Naye akaondoka huko akaenda Mlima Karmeli, na kutoka huko akarudi Samaria.

Copyright information for Neno