2 Kings 21

Manase Mfalme Wa Yuda

1Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, akatawala katika Yerusalemu kwa miaka hamsini na mitano. Jina la mama yake aliitwa Hefsiba. 2Akafanya maovu machoni pa BWANA, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo BWANA aliyafukuza mbele ya Waisraeli. 3Akajenga tena mahali pa juu pa kuabudia miungu ambapo baba yake Hezekia alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akasujudia na kuabudu jeshi lote la angani. 4Akajenga madhabahu ndani ya Hekalu la BWANA, ambalo BWANA alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.” 5Katika nyua zote mbili za Hekalu la BWANA, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. 6Akamtoa kafara mwanawe mwenyewe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa BWANA na kumghadhibisha.

7Akachukua nguzo ya Ashera aliyoitengeneza na kuiweka ndani ya Hekalu, ambalo BWANA alikuwa amemwambia Daudi na Solomoni mwanawe hivi, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu, ambavyo nimevichagua kutoka katika makabila yote ya Israeli, nitaliweka Jina langu milele. 8Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli itangetange kutoka katika nchi niliyowapa baba zao, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru na kuishika Sheria yote ambayo walipewa na Mose mtumishi wangu.” 9Lakini hawa watu hawakusikiliza. Manase akawapotosha, hivyo kwamba walifanya maovu mengi zaidi kuliko mataifa yale ambayo BWANA aliwaangamiza mbele ya Waisraeli.

10BWANA akasema kupitia watumishi wake manabii: 11“Manase mfalme wa Yuda ametenda dhambi hizi za kuchukiza. Amefanya maovu mengi kuliko Waamori waliokuwepo kabla yake na ameiongoza Yuda katika dhambi kwa sanamu zake. 12Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Nitaleta maafa makubwa juu ya Yerusalemu na Yuda kiasi kwamba masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yatawasha. 13Nitanyosha juu ya Yerusalemu kamba ya kupimia iliyotumika dhidi ya Samaria na timazi iliyotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu. Nitaifutilia mbali Yerusalemu kama mtu afutaye sahani, nikiifuta na kuifunikiza. 14Nitawakataa mabaki wa urithi wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao. Watapokonywa mali zao na kutekwa nyara na adui zao wote, 15kwa sababu wametenda uovu machoni pangu na kunighadhibisha tangu siku baba zao walipotoka Misri mpaka siku ya leo.”

16Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, hivyo kwamba wakatenda maovu machoni pa BWANA.

17Matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda? 18Manase akalala pamoja na baba zake na akazikwa katika bustani ya jumba la mfalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Amoni Mfalme Wa Yuda

19Amoni alikuwa na miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala, akatawala katika Yerusalemu kwa miaka miwili. Jina la mama yake aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, alitoka Yotba. 20Akatenda maovu machoni mwa BWANA, kama baba yake Manase alivyofanya. 21Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia. 22Akamwacha BWANA, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za BWANA.

23Maafisa wa Amoni wakafanya shauri baya dhidi yake, nao wakamwua mfalme katika jumba lake la kifalme. 24Kisha watu wa nchi wakawaua wote waliopanga hilo shauri baya dhidi ya Mfalme Amoni, nao wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.

25Matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu cha wafalme wa Yuda? 26Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Yosia mwanawe akaingia mahali pake kuwa mfalme.

Copyright information for Neno