2 Kings 4

Mafuta Ya Mjane

Mke wa mtu mmoja kutoka katika wana wa manabii akamwendea Elisha, akamwambia, “Mtumishi wako mume wangu amekufa, nawe unajua alikuwa anamcha BWANA. Lakini sasa yule anayemdai anakuja kuchukua wanangu wawili kama watumwa wake.”

Elisha akamjibu, “Nitawezaje kukusaidia? Niambie, una nini ndani ya nyumba yako?”

Akasema, “Mtumishi wako hana kitu cho chote kabisa isipokuwa mafuta kidogo.”

Elisha akasema, “Zunguka kwa majirani zako wote ukaombe vyombo vitupu. Usiombe vichache. Kisha ingia ndani na ujifungie mlango wewe na wanao. Mimina mafuta kwenye vyombo vyote, kila kimoja kinapojaa, kiweke kando.”

Yule mjane akaondoka na kujifungia ndani, yeye na wanawe. Wao wakamletea vyombo naye akaendelea kumimina mafuta. Vyombo vyote vilipojaa, akamwambia mwanawe, “Niletee chombo kingine.”

Lakini mwanawe akajibu, “Hakuna chombo kingine kilichobaki.” Basi mafuta yakakoma kutiririka.

Yule mwanamke akamwendea yule mtu wa Mungu, naye mtu wa Mungu akasema, “Nenda ukayauze hayo mafuta ulipe madeni yako. Wewe na wanao mnaweza kuishi kwa kile kinachosalia.”

Mwana Wa Mshunami Afufuliwa

Siku moja Elisha akaenda Shunemu. Huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye uwezo, ambaye alimsisitiza Elisha aje kula chakula. Kwa hiyo kila mara alipokuja, alipitia pale ili ale. Akamwambia mumewe, “Ninajua kwamba huyu mtu ambaye anakuja kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. 10 Tutengeneze chumba kidogo juu darini na tuweke ndani yake kitanda na meza, kiti na taa kwa ajili yake. Kisha anaweza kukaa humo kila mara akija kwetu.”

11 Siku moja Elisha alipokuja, akapanda chumbani kwake na kulala humo. 12 Akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Mwite huyo Mshunami.” Hivyo akamwita naye akaja akasimama mbele yake. 13 Elisha akamwambia mtumishi wake, “Mwambie huyu mwanamke, umetaabika sana kwa ajili yetu. Sasa utendewe nini? Je, tunaweza kuzungumza na mfalme au jemadari wa jeshi kwa niaba yako?”

Akajibu, “Mimi nina kwangu miongoni mwa watu wangu.”

14 Elisha akamwambia mtumishi wake, “Je, ni nini kinachoweza kufanyika kwa ajili yake?”

Gehazi akasema, “Vyema, hana mwana na mume wake ni mzee.”

15 Ndipo Elisha akasema, “Mwite huyo mwanamke.” Kwa hiyo akamwita, naye akaja akasimama mlangoni. 16 Elisha akamwambia, “Mwaka ujao, wakati kama huu utabeba mwana mikononi mwako.”

Yule mama akapinga, akasema, “La hasha, bwana wangu, usimpotoshe mtumishi wako, Ee mtu wa Mungu!”

17 Lakini yule mwanamke akapata mimba, na mwaka uliofuata wakati kama ule ule akamzaa mwana, kama vile Elisha alivyokuwa amemwambia.

18 Mtoto akakua, naye siku moja akamwendea baba yake, ambaye alikuwa pamoja na wavunaji. 19 Akamwambia baba yake, “Kichwa changu! Kichwa changu!”

Baba yake akamwambia mtumishi, “Mchukue umpeleke kwa mama yake.”
20 Baada ya mtumishi kumbeba na kumpeleka kwa mama yake, mtoto akaketi mapajani mwa mama yake mpaka adhuhuri, kisha akafa. 21 Mama akampandisha na kumlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, kisha akafunga mlango, akatoka nje.

22 Akamwita mume wake na kusema, “Tafadhali mtume mmoja miongoni mwa mtumishi pamoja na punda ili niweze kwenda kwa mtu wa Mungu haraka na kurudi.”

23 Mume wake akamwuliza, “Kwa nini kwenda kwake leo? Leo si mwandamo wa mwezi, wala si Sabato.”

Mwanamke akasema, “Yote ni sawa.”

24 Akatandika punda na kumwambia mtumishi wake, “Mwongoze huyo punda, usinipunguzie mwendo mpaka nikuambie.” 25 Kwa hiyo akaenda na kumfikia huyo mtu wa Mungu katika Mlima Karmeli.

Alipomwona kwa mbali, huyo mtu wa Mungu akamwambia mtumishi wake Gehazi, “Tazama, yule Mshunami!
26 Kimbia ukamlaki na umwulize, ‘Je, wewe hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto wako ni mzima?’ ”

Akasema, “Kila kitu ni sawasawa.”

27 Alipomfikia huyo mtu wa Mungu pale mlimani, akashika miguu yake. Gehazi akaja ili amwondoe, lakini yule mtu wa Mungu akasema, “Mwache! Yuko katika uchungu mkubwa, lakini BWANA amenificha jambo hili na hajaniambia kwa nini.”

28 Yule mwanamke akasema, “Je, bwana wangu, mimi nilikuomba mwana? Je, sikukuambia, ‘Usiamshe matumaini yangu’?”

29 Elisha akamwambia Gehazi, “Jikaze viuno, chukua fimbo yangu mkononi mwako na ukimbie. Ikiwa utakutana na mtu ye yote, usimsalimie, na mtu ye yote akikusalimu, usimjibu. Ilaze fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.”

30 Lakini mama wa mtoto akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo na wewe uishivyo, sitakuacha.” Kwa hiyo Elisha akainuka, akafuatana naye.

31 Gehazi akatangulia mbele na kuilaza fimbo juu ya uso wa mtoto, lakini hapakuwa na sauti wala itikio. Hivyo Gehazi akarudi kukutana na Elisha, na kumwambia, “Mtoto hajaamka.”

32 Elisha alipofika kwenye ile nyumba, mtoto alikuwa amelala juu ya kitanda chake angali amekufa. 33 Akaingia ndani, akajifungia yeye na yule mtoto, akamwomba BWANA. 34 Kisha akapanda kitandani, akalala juu ya yule mtoto, mdomo wake juu ya mdomo wa mtoto, macho yake juu ya macho ya mtoto, mikono yake juu ya mikono ya mtoto. Naye alipojinyosha juu yake, mwili wa mtoto ukapata joto. 35 Elisha akajiondoa juu yake na kuanza kutembeatembea ndani ya chumba na kisha akarudi tena kitandani na kujinyosha tena juu ya mtoto mara nyingine. Mtoto akapiga chafya mara saba na akafungua macho yake.

36 Elisha akamwita Gehazi na kumwambia, “Mwite huyo Mshunami.” Naye akafanya hivyo. Yule Mshunami alipokuja, Elisha akasema, “Mchukue mwanao.” 37 Akaingia ndani, akaanguka miguuni pa Elisha na kusujudu hadi nchi. Kisha akamchukua mwanawe na kutoka nje.

Mauti Ndani Ya Chungu

38 Elisha akarudi Gilgali nako huko kulikuwa na njaa katika eneo lile. Wakati wana wa kundi la manabii walipokuwa wanakutana naye, akamwambia mtumishi wake, “Teleka chungu kikubwa jikoni uwapikie manabii.”

39 Mmoja wao akatoka kwenda mashambani kuchuma mboga na akapata mtango mwitu. Akachuma matango na kujaza nguo yake aliyoikunja ili kubebea. Aliporudi, akayakatakata na kuyatumbukiza ndani ya chungu, ingawa hakuna aliyejua ni nini. 40 Mchuzi ukagawiwa watu, lakini walipoanza kula, wakalia, “Ee mtu wa Mungu, kuna mauti ndani ya chungu.” Nao hawakuweza kula.

41 Elisha akasema, “Leteni unga.” Akauweka ndani ya chungu na kusema, “Wagawie watu ili wale.” Wala hapakuwa na kitu cho chote chenye madhara ndani ya chungu.

Watu Mia Wanalishwa

42 Akaja mtu kutoka Baal-Shalisha, akimletea mtu wa Mungu mikate ishirini ya shayiri iliyookwa kutokana na nafaka ya kwanza, pamoja na masuke ya nafaka mpya. Elisha akasema, “Wape watu ili wale”

43 Mtumishi wake akamwuliza, “Nitawezaje kuandaa hii mbele ya watu mia?”

Lakini Elisha akajibu, “Wape watu ili wale. Kwa maana hivi ndivyo asemavyo BWANA: ‘Watakula na kusaza.’ ”
44 Basi akaiandaa mbele yao ile mikate, wakala na baadhi yake wakasaza, sawasawa na neno la BWANA.

Copyright information for Neno