2 Samuel 10

Daudi Awashinda Waamoni

1Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akaingia mahali pake. 2Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma ujumbe kuonyesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake.

Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni,
3wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonyesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?” 4Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaacha waende zao.

5Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko mpaka ndevu zenu zikishakuwa ndipo mje.”

6Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa harufu mbaya kwenye pua za Daudi, wakaajiri askari wa miguu 20,000 wa Kiaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka pamoja na watu 1,000, na vile vile watu 12,000 kutoka Tobu.

7Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. 8Waamoni wakatoka wakajipanga kwenye vita penye ingilio la lango la mji wao, wakati Waaramu wa Soba, wa Rehobu, watu wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi.

9Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; hivyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu. 10Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni. 11Yoabu akasema, “Ikiwa Waaramu wana nguvu kunizidi, basi itawabidi mje kuniokoa, lakini ikiwa Waamoni wana nguvu kuwazidi ninyi, basi nitakuja kuwaokoa. 12Iweni hodari na tupigane kishujaa kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. BWANA atafanya lile lililo jema machoni pake.”

13Basi Yoabu na vikosi vyake wakatangulia mbele kupigana na Waaramu, nao wakakimbia mbele yake. 14Waamoni walipoona kwamba Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu.

15Baada ya Waaramu kuona wamekimbizwa na Israeli, wakajikusanya tena. 16Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ng'ambo ya Mto Eufrati, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza.

17Daudi alipoambiwa jambo hili, akakusanya Israeli yote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi. 18Lakini wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akaua watu wao mia saba wapanda magari yao ya vita na askari wao wa miguu 40,000. Vile vile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko. 19Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao.

Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.

Copyright information for Neno