2 Samuel 21

Wagibeoni Wanalipiza Kisasi

1Wakati wa utawala wa Daudi kulikuwa na njaa kwa miaka mitatu mfululizo, kwa hiyo Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, “Ni kwa sababu ya Sauli na nyumba yake iliyotiwa madoa ya damu, kwa sababu aliwaua Wagibeoni.”

2Mfalme akawaita Wagibeoni na kuzumgumza nao. (Wagibeoni hawakuwa wa wana wa Israeli, ila walikuwa mabaki ya Waamori. Waisraeli walikuwa wameapa kuwaacha hai, lakini Sauli katika wivu wake kwa ajili ya Israeli na Yuda, alikuwa amejaribu kuwaangamiza.) 3Daudi akawauliza Wagibeoni, “Niwatendee nini? Nitawaridhishaje ili mbariki urithi wa BWANA?”

4Wagibeoni wakamjibu, “Hatuna haki ya kudai fedha wala dhahabu kutoka kwa Sauli au jamaa yake, wala hatuna haki ya kumwua mtu ye yote katika Israeli.”

Daudi akawauliza, “Mnataka niwafanyie nini?”

5Wakamjibu mfalme, “Kwa habari ya mtu aliyetuangamiza na kufanya hila mbaya dhidi yetu ili kwamba tuangamizwe na tusiwe na ye yote katika Israeli, 6tupatieni wazao wake saba wa kiume tuwaue hadharani mbele za BWANA huko Gibea ya Sauli, aliyekuwa amechaguliwa na BWANA.”

Basi mfalme akasema, “Nitawakabidhi kwenu.”

7Mfalme akamhifadhi Mefiboshethi mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa sababu ya kile kiapo mbele za BWANA kati ya Daudi na Yonathani. 8Lakini mfalme akamchukua Armoni na Mefiboshethi, wana wawili wa Rispa binti Ahiya, ambao alikuwa amemzalia Sauli, pamoja na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliokuwa amemzalia Adrieli mwana wa Barzilai, Mmeholathi. 9Akawakabidhi kwa Wagibeoni, ambao waliwaua na kuwaweka wazi juu ya kilima mbele za BWANA. Wote saba walianguka kwa pamoja; waliuawa katika siku za kwanza za mavuno, mara tu uvunaji wa shayiri ulipokuwa unaanza.

10Rispa binti Ahiya akachukua nguo ya gunia, akajitandikia juu ya mwamba. Kuanzia mwanzo wa mavuno mpaka mvua ziliponyesha juu ya miili ya hao waliouawa, Rispa hakuruhusu ndege wa angani kuwagusa wakati wa mchana, wala wanyama wa mwitu wakati wa usiku. 11Daudi alipoambiwa kile Rispa binti Ahiya, suria wa Sauli, alichokuwa amekifanya, 12alikwenda akachukua mifupa ya Sauli na mwanawe Yonathani kutoka kwa watu wa Yabeshi-Gileadi. (Walikuwa wameichukua kwa siri kutoka katika uwanja wa watu wote huko Beth-Shani, mahali ambapo Wafilisti walikuwa wamewatundika baada ya kumwua Sauli huko Gilboa.) 13Daudi akaileta mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani kutoka huko, pia mifupa ya wale ambao walikuwa wameuawa na kutupwa ilikusanywa.

14Wakazika mifupa ya Sauli na ya mwanawe Yonathani katika kaburi la Kishi, babaye Sauli, huko Sela katika nchi ya Benyamini, nao wakafanya kila kitu mfalme alichoagiza. Baada ya hayo, Mungu akajibu maombi kwa ajili ya nchi.

Vita Dhidi Ya Wafilisti

15Kwa mara nyingine tena kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Israeli. Daudi akashuka pamoja na watu wake ili kupigana dhidi ya Wafilisti, naye akawa amechoka sana. 16Naye Ishbi-Benobu, mmoja wa wazao wa Warefai
21.16 Yaani majitu
, ambaye mkuki wake ulikuwa na uzito wa shekeli 300 za shaba
21.16 Shekeli 300 za shaba ni sawa na kilo 3.5
, alikuwa amejifunga upanga mpya, naye alisema angemwua Daudi.
17Lakini Abishai mwana wa Seruya akaja kumwokoa Daudi; akampiga huyo Mfilisti, akamwangusha chini na kumwua. Ndipo watu wakamwapia Daudi, wakisema, “Kamwe hutakwenda tena nasi vitani, ili kwamba taa ya Israeli isije ikazimwa.”

18Baada ya muda, kukawa na vita nyingine na Wafilisti, huko Gobu. Wakati huo Sibekai, Mhushathi, akamwua Safu, mmoja wa wazao wa Warefai.

19Katika vita nyingine na Wafilisti huko Gobu, Elhanani mwana wa Yaare-Oregimu, Mbethlehemu, alimwua nduguye Goliathi, Mgiti, ambaye mkuki wake ulikuwa na mpini kama mti wa mfumaji.

20Katika vita vingine tena, vilivyopiganwa huko Gathi, kulikuwako jitu kubwa sana refu lililokuwa na vidole sita katika kila mkono na vidole sita kila mguu, jumla vidole ishirini na vinne. Vile vile alikuwa mzao wa Warefai. 21Alipowadhihaki Israeli, Yonathani mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua.

22Hawa wanne walikuwa wazao wa Warefai katika Gathi, nao walianguka katika mikono ya Daudi na watu wake.

Copyright information for Neno