2 Samuel 22

Wimbo Wa Daudi Wa Sifa

Daudi akamwimbia BWANA maneno ya wimbo huu hapo BWANA alipomwokoa kutoka katika mkono wa adui zake wote, pia kutoka katika mkono wa Sauli. Akasema: “BWANA ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
Mungu wangu ni mwamba wangu,
ambaye kwake nakimbilia,
ngao yangu na pembe ya wokovu wangu.
Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu
na mwokozi wangu,
huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
Namwita BWANA, yeye anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa
kutoka kwa adui zangu.
“Mawimbi ya mauti yalinizunguka,
maji mengi ya ghafula
ya uharibifu yalinifunika.
Kamba za kuzimu
22.6 Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, maana yake ni Shimo lisilo na mwisho
zilinizunguka,
mitego ya kifo ilinikabili.
Katika shida yangu nilimwita BWANA,
nilimwita Mungu wangu.
Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika masikioni mwake.
“Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya mbingu ilitikisika,
vilitetemeka kwa sababu
alikuwa amekasirika.
Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto ulao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yawakayo kwa nguvu
yalitoka humo.
10 Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
11 Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mbawa za upepo.
12 Alifanya giza kuwa kitu chake cha kujifunika:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
13 Kutokana na mng'ao wa uwepo wake
mawingu yalisogea,
ikanyesha mvua ya mawe
na umeme wa radi.
14 BWANA alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
15 Aliipiga mishale akatawanya adui,
umeme wa radi na kuwakimbiza.
16 Mabonde ya bahari yalifunuliwa
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwake BWANA,
kwa uvumi wa pumzi
kutoka puani mwake.
17 “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka katika kilindi
cha maji makuu.
18 Aliniokoa kutoka mtesi wangu
mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu, waliokuwa na nguvu
nyingi kuliko mimi.
19 Walinikabili katika siku ya msiba wangu,
lakini BWANA alikuwa msaada wangu.
20 Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa sababu alipendezwa nami.
21 “BWANA alinitendea kwa kadiri ya uadilifu wangu;
kwa kadiri ya usafi wa mikono yangu amenilipa.
22 Kwa maana nimezishika njia za BWANA
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
23 Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
24 Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
25 BWANA amenilipa sawa sawa na uadilifu wangu,
sawa sawa na usafi wangu machoni pake.
26 “Kwa yeye aliye mwaminifu
unajionyesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia unajionyesha
kuwa asiye na hatia,
27 kwa aliye mtakatifu
unajionyesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka
unajionyesha kuwa mkaidi.
28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi
ili uwashushe.
29 Wewe ni taa yangu, Ee BWANA.
BWANA hulifanya giza langu
kuwa mwanga.
30 Kwa msaada wako naweza kusogeza jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka.
31 “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu;
neno la BWANA ni kamilifu.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
32 Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya BWANA?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
33 Mungu ndiye anivikaye nguvu
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
34 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
35 Huifundisha mikono yangu kwa ajili ya kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upindi wa shaba.
36 Hunipa ngao yako ya ushindi,
hujishusha chini ili kuniinua.
37 Huyapanua mapito yangu,
ili vifundo vya miguu yangu visipinduke.
38 “Nilifuatia adui zangu na nikawaseta;
sikurudi nyuma mpaka walipoangamizwa.
39 Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka;
walianguka chini ya miguu yangu.
40 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu
kusujudu miguuni pangu.
41 Uliwafanya adui zangu wageuke na wakakimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
42 Walipiga yowe, lakini hapakuwapo na ye yote wa kuwaokoa;
walimlilia BWANA, lakini hakuwajibu.
43 Niliwapiga wakawa laini kama mavumbi ya nchi;
nikawaponda na kuwakanyaga
kama tope barabarani.
44 “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu;
umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa.
Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
45 nao wageni huja wakininyenyekea;
mara wanisikiapo, hunitii.
46 Wote hulegea;
huja wakitetemeka
kutoka kwenye ngome zao.
47 “BWANA yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu,
Mwamba, Mwokozi wangu!
48 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
ayawekaye mataifa chini yangu,
49 aniwekaye huru toka kwa adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
50 Kwa hiyo nitakusifu wewe, Ee BWANA,
katikati ya mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.
51 Humpa mfalme wake ushindi mkuu;
huonyesha fadhili zake
kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.”


Copyright information for Neno