2 Samuel 5

Daudi Awa Mfalme Juu Ya Israeli

1Makabila yote ya Israeli yakamjia Daudi huko Hebroni na kumwambia, “Sisi tu nyama yako na damu yako hasa. 2Zamani, wakati Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ulikuwa ndiye uliyeongoza Israeli vitani. Naye BWANA akakuambia, ‘Utawachunga watu wangu Israeli, nawe utakuwa kiongozi wao.’ ”

3Wazee wote wa Israeli wakamwendea Mfalme Daudi huko Hebroni, mfalme akafanya mapatano nao huko Hebroni mbele za BWANA, nao wakamtia Daudi mafuta kuwa mfalme wa Israeli.

4Daudi alikuwa na miaka thelathini alipoanza kutawala, naye akatawala Israeli miaka arobaini. 5Huko Hebroni alitawala Yuda kwa miaka saba na miezi sita, na katika Yerusalemu alitawala Israeli yote na Yuda kwa miaka thelathini na mitatu.

Daudi Anashinda Yerusalemu

6Mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi walioishi huko. Wayebusi wakamwambia Daudi, “Hutaingia hapa ndani, kwani hata vipofu na viwete wanaweza kukufukuza.” Walidhani, “Daudi hawezi kuingia humu.” 7Hata hivyo, Daudi akateka ngome ya Sayuni, Mji wa Daudi.

8Siku ile, Daudi akasema, “Ye yote ambaye atawashinda Wayebusi, atatumia huo mfereji kuwafikia hao ‘viwete na vipofu’ ambao ni adui za Daudi.” Ndiyo sababu wanasema, “ ‘Vipofu na viwete’ hawataingia kwenye jumba la ufalme.”

9Ndipo Daudi akafanya makao ndani ya ngome na kuiita Mji wa Daudi. Akajenga eneo linalozunguka kuanzia Milo
5:9 Milo maana yake Boma la Ngome
kuelekea ndani.
10Daudi akazidi kuwa na mamlaka zaidi na zaidi, kwa sababu BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote alikuwa pamoja naye.

11Basi Hiramu mfalme wa Tiro akatuma wajumbe kwa Daudi, pamoja na magogo ya mierezi, maseremala na waashi, nao wakajenga jumba la kifalme kwa ajili ya Daudi. 12Naye Daudi akafahamu kuwa BWANA amemwimarisha kama mfalme juu ya Israeli na ameinua ufalme wake kwa ajili ya Israeli watu wake.

13Baada ya Daudi kuondoka Hebroni, akajitwalia masuria zaidi na wake huko Yerusalemu, nao wana na binti wengi walizaliwa kwake. 14Haya ndiyo majina ya watoto waliozaliwa kwake huko: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, 15Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia, 16Elishama, Eliada na Elifeleti.

Daudi Awashinda Wafilisti

17Wafilisti waliposikia kuwa Daudi ametiwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wakapanda kwa nguvu zote kumtafuta, lakini Daudi akasikia kuhusu jambo hili akatelemka kwenye ngome. 18Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kusambaa kwenye Bonde la Refaimu, 19kwa hiyo Daudi akamwuliza BWANA, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?”

BWANA akamjibu, “Nenda, kwa maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.”

20Ndipo Daudi akaenda mpaka Baal-Perasimu na huko akawashinda Wafilisti. Akasema, “Kama mafuriko yafurikavyo, BWANA amewafurikia adui zangu mbele yangu.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-Perasimu
5.20 Maana yake Bwana Afurikae
.
21Wafilisti wakatelekeza vinyago vyao huko, naye Daudi na watu wake wakavichukua.

22Wafilisti walikwea kwa mara nyingine tena na kusambaa katika Bonde la Refaimu. 23Kwa hiyo Daudi akamwuliza BWANA, naye akamjibu, “Usipande moja kwa moja, bali wazungukie kwa nyuma na uwashambulie mbele ya miti ya miforosadi. 24Mara utakaposikia sauti ya kutembea kutoka kwenye vilele vya miti ya miforosadi, nenda haraka, kwa sababu hiyo itamaanisha kuwa BWANA ametangulia mbele yako kupiga jeshi la Wafilisti.” 25Basi Daudi akafanya kama BWANA alivyomwagiza, naye akawaangusha Wafilisti njia yote kuanzia Gebba
5.25 Kwa Kiebrania mji huu uliitwa Gibeoni (ona 1 Nya 14:16)
hadi Gezeri.

Copyright information for Neno