2 Samuel 7

Ahadi Ya Mungu Kwa Daudi

1Baada ya mfalme kukaa katika jumba lake la kifalme kwa utulivu, naye BWANA akiwa amemstarehesha pande zote mbali na adui zake, 2akamwambia nabii Nathani, “Mimi hapa, ninaishi katika jumba la kifalme la mierezi, wakati Sanduku la Mungu limebaki katika hema.”

3Nathani akamjibu mfalme, “Lo lote ulilo nalo moyoni, endelea ukalifanye, kwa maana BWANA yu pamoja nawe.”

4Usiku ule neno la BWANA likamjia Nathani, kusema:

5“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo BWANA asemalo: Je, ewe ndiwe wa kunijengea mimi nyumba ili nikae ndani yake? 6Sijakaa ndani ya nyumba tangu siku niliyowaleta Waisraeli kutoka Misri hadi leo. Nimekuwa nikitembea kutoka mahali pamoja hadi mahali pengine ndani ya hema kama makao yangu. 7Po pote nilipotembea pamoja na Waisraeli wote, je, nimewahi kumwambia kiongozi wao ye yote niliyemwamuru kuwachunga watu wangu Israeli, “Kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?” ’

8“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo BWANA Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nilikutoa wewe kutoka machungani na kutoka kuandama kundi la kondoo na mbuzi ili kuwaongoza watu wangu Israeli. 9Nimekuwa pamoja nawe po pote ulipokwenda, nami nimekatilia mbali adui zako wote mbele ya uso wako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya walio wakuu sana wa dunia. 10Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali niwapande humo ili kwamba wawe na nyumbani kwao wenyewe wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni, 11na kama walivyofanya tangu mwanzo wakati nilipowaweka viongozi juu ya watu wangu Israeli. Pia nitawapa raha mbele ya adui zenu wote.

“ ‘BWANA akuambia kwamba BWANA mwenyewe atakujengea nyumba.
12Siku zako zitakapokwisha nawe ulale pamoja na baba zako, nitainua mzao wako aingie mahali pako, ambaye atatoka viunoni mwako, nami nitauimarisha ufalme wake. 13Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, nami nitaimarisha kiti cha enzi cha ufalme wake milele. 14Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Atakapokosea nitamwadhibu kwa fimbo ya wanadamu, kwa adhabu ya kupigwa na wanadamu. 15Lakini upendo wangu kamwe hautaondolewa kwake, kama nilivyouondoa kwa Sauli, niliyemwondoa atoke mbele yako. 16Nyumba yako na ufalme wako utadumu milele mbele zangu, kiti chako cha enzi kitafanywa imara milele.’ ”17Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

Maombi Ya Daudi

18Basi Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za BWANA, akasema:

“Ee BWANA Mwenyezi, mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini, hata umenileta mpaka hapa nilipo?
19Naam, kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee BWANA Mwenyezi, wewe umenena pia habari za wakati ujao kuhusu nyumba ya mtumishi wako. Je, hii ndiyo njia yako ya kawaida ya kushughulika na mwanadamu, Ee BWANA Mwenyezi?

20“Je, Daudi aweza kukuambia nini zaidi? Kwa maana unamjua mtumishi wako, Ee BWANA Mwenyezi. 21Kwa ajili ya neno lako na kwa mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa na kulifanya lijulikane na lifahamike kwa mtumishi wako.

22“Tazama jinsi ulivyo mkuu, Ee BWANA Mwenyezi! Hakuna mwingine kama wewe, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe, 23Ni nani aliye kama watu wako Israeli, taifa pekee duniani ambalo Mungu alitoka kwenda kulikomboa kuwa taifa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina mwenyewe na kufanya mambo makuu na maajabu ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa na miungu yao kutoka mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri? 24Umeimarisha watu wako Israeli hasa kama watu wako mwenyewe milele, nawe, Ee BWANA, umekuwa Mungu wao.

25“Basi sasa, BWANA, ukaitimize ahadi uliyosema kuhusu mtumishi wako na nyumba yake milele. Ukafanye kama ulivyoahidi, 26ili kwamba jina lako litukuke milele. Ndipo watu watasema, ‘BWANA Mwenye Nguvu Zote ni Mungu juu ya Israeli!’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itakuwa imara mbele zako.

27“Ee BWANA Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, umelifunua hili kwa mtumishi wako, ukisema, ‘Nitakujengea nyumba.’ Hivyo mtumishi wako amepata ujasiri kukuletea dua hii. 28Ee BWANA Mwenyezi, wewe ndiwe Mungu! Maneno yako ndiyo kweli, nawe umeahidi mambo haya mazuri kwa mtumishi wako. 29Sasa naomba uwe radhi kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili iweze kudumu mbele zako milele, kwa maana wewe, Ee BWANA Mwenyezi, umesema, na kwa baraka zako nyumba ya mtumishi wako itaendelea kubarikiwa milele.”

Copyright information for Neno