2 Samuel 13

Amnoni Na Tamari

1Ikawa baada ya hayo, Amnoni mwana wa Daudi akampenda Tamari, umbu lake Absalomu mwana wa Daudi, ambaye alikuwa mzuri wa sura.

2Amnoni akasumbuka sana kuhusu Tamari hata akaugua, kwa kuwa Tamari alikuwa bikira, na ilionekana kwamba haiwezekani Amnoni kumfanyia jambo lo lote.

3Basi Amnoni alikuwa na rafiki jina lake Yonadabu mwana wa Shimea
13.3 Shimea pia hutamkwa Shama
, nduguye Daudi. Yonadabu alikuwa mtu wa hila nyingi sana.
4Akamwuliza Amnoni, “Wewe ni mtoto wa mfalme; kwa nini siku baada ya siku unaonekana kukonda? Hutaniambia?”

Amnoni akamwambia, “Ninampenda Tamari, dada yake Absalomu ndugu yangu.”

5Yonadabu akamwambia, “Nenda ukalale kitandani na ujifanye kuwa mgonjwa. Baba yako atakapokuja kukuona mwambie, ‘Ningependa Tamari dada yangu aje kunipatia cho chote ili nile. Tafadhali mruhusu aje na kuniandalia chakula mbele yangu ningali ninamwona, ili nipate kula kutoka mkononi mwake.’ ”

6Kwa hiyo Amnoni akalala kitandani kujifanya mgonjwa. Mfalme alipokuja kumwona, Amnoni akamwambia, “Ningependa dada yangu Tamari aje na kuniandalia mikate maalum mbele yangu, ili nipate kula toka mkononi mwake.”

7Daudi akampelekea Tamari ujumbe huko kwenye jumba la kifalme, kusema: “Nenda katika nyumba ya ndugu yako Amnoni ukamwandalie chakula.” 8Kwa hiyo Tamari akaenda nyumbani kwa nduguye Amnoni, ndugu ambaye alikuwa amelala. Tamari akachukua unga uliotiwa hamira akaukanda, akaiandaa mikate mbele yake na kuioka. 9Tamari akaondoa mikate kwenye kikaango ili ampatie Amnoni, lakini akakataa kula.

Amnoni akamwambia, “Mtoe nje kila mtu aliyeko hapa.” Kwa hiyo kila mmoja akaondoka.
10Ndipo Amnoni akamwambia Tamari, “Leta mkate hapa ndani ya chumba changu ili nipate kula kutoka mkononi mwako.” Basi Tamari akachukua mikate aliyoiandaa na kumletea Amnoni ndugu yake ndani ya chumba chake. 11Lakini alipompelekea ili ale, akamkamata kwa nguvu na kumwambia, “Njoo ulale nami, dada yangu.”

12Akamwambia, “Usifanye hivyo, ndugu yangu! Usinitende jeuri! Jambo la namna hii halistahili kufanyika katika Israeli! Usitende jambo hili ovu. 13Kwa upande wangu je, itakuwaje? Nitaipeleka wapi aibu yangu? Pia kwa upande wako, itakuwaje? Utakuwa kama mmoja wa wapumbavu waovu katika Israeli. Tafadhali zungumza na mfalme; hatakukatalia wewe kunioa,” 14Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza, na kwa kuwa alikuwa na nguvu kuliko Tamari, akamtenda jeuri.

15Kisha Amnoni akamchukia Tamari, kwa machukio makuu sana. Kwa kweli, Amnoni alimchukia kuliko alivyokuwa amempenda. Amnoni akamwambia, “Inuka na utoke nje!”

16Tamari akamwambia, “Hapana! Kunifukuza itakuwa vibaya zaidi kuliko yale uliyonitendea.”

Lakini Amnoni akakataa kumsikiliza.
17Akamwita mtumishi wake mahsusi na kumwambia, “Mtoe huyu mwanamke hapa na ufunge mlango nyuma yake.” 18Kwa hiyo, mtumishi wake akamtoa nje na kufunga mlango nyuma yake. Tamari alikuwa amevaa joho lililopambwa vizuri, kwa maana lilikuwa ndilo aina ya vazi lililovaliwa na binti za kifalme walio mabikira. 19Tamari akajitia majivu kichwani mwake na kurarua lile joho alilokuwa amevaa. Akaweka mkono wake kichwani akaenda zake akilia kwa sauti.

20Absalomu nduguye akamwuliza, “Je, huyo Amnoni ndugu yako, amekutana nawe kimwili? Sasa nyamaza umbu langu, yeye ni ndugu yako. Usilitie jambo hili moyoni.” Naye Tamari akaishi nyumbani kwa Absalomu nduguye, akiwa mwanamke mwenye huzuni.

21Mfalme Daudi aliposikia mambo haya yote, akakasirika sana. 22Absalomu hakusema neno lo lote na Amnoni, likiwa zuri au baya, kwa kuwa alimchukia Amnoni kwa sababu alikuwa amemtia aibu Tamari, dada yake.

Absalomu Amuua Amnoni

23Miaka miwili baadaye, wakati wakata manyoya ya kondoo wa Absalomu walipokuwa huko Baal-Hasori karibu na mpaka wa Efraimu, alialika wana wote wa mfalme kuja huko. 24Absalomu akaenda kwa mfalme na kumwambia, “Mtumishi wako ninao wakata kondoo manyoya waliokuja. Tafadhali, je, mfalme na maafisa wake wanaweza kuungana nami?”

25Mfalme akajibu, “La hasha, mwanangu si lazima sisi sote tuje, tutakuwa tu mzigo kwako.” Ingawa Absalomu alimsihi sana, mfalme alikataa kwenda, lakini alimbariki.

26Basi Absalomu akasema, “Kama hutakuja, tafadhali mruhusu ndugu yangu Amnoni twende pamoja naye.”

Mfalme akamwuliza, “Kwa nini aende pamoja nawe?”
27Lakini Absalomu alimsihi, kwa hiyo mfalme akamtuma Amnoni pamoja na wana wengine wa mfalme waliobaki.

28Absalomu aliagiza watu wake, “Sikilizeni! Wakati Amnoni atakapokuwa amekunywa mvinyo na kulewa sana nami nikiwaambia, ‘Mpigeni Amnoni,’ basi mwueni. Msiogope. Je, si mimi niliyewapa amri hii? Iweni hodari na wenye ushujaa.” 29Kwa hiyo watu wa Absalomu wakamtendea Amnoni kama vile Absalomu alivyokuwa amewaagiza. Ndipo wana wote wa mfalme wakainuka, wakapanda nyumbu zao, wakakimbia.

30Wakati wakiwa njiani, taarifa ilimjia Daudi, kusema: “Absalomu amewaua wana wote wa mfalme; hakuna hata mmoja aliyesalia.” 31Mfalme akasimama, akararua nguo zake, akalala chini ardhini; nao watumishi wake wote wakasimama kando yake na nguo zao zikiwa zimeraruliwa.

32Lakini Yonadabu mwana wa Shimea, nduguye Daudi, akasema, “Bwana wangu asifikiri kwamba wamewaua wana wote wa mfalme; ni Amnoni peke yake ndiye aliyekufa. Hili limekuwa kusudi la moyo wa Absalomu tangu siku ile Amnoni alipomtendea jeuri Tamari, dada yake. 33Mfalme bwana wangu asisumbuliwe na taarifa kwamba wamewaua wana wote wa mfalme. Ni Amnoni peke yake aliyekufa.”

34Wakati huo, Absalomu akawa amekimbia.

Basi mlinzi akaangalia, naye akaona watu wengi barabarani magharibi yake, wakishuka kutoka upande wa kilima. Mlinzi akaenda akamwambia mfalme, “Naona watu wakitokea upande wa Horonaimu, huko upande wa kilimani.”

35Yonadabu akamwambia mfalme, “Tazama, wana wa mfalme wako hapa; imekuwa kama vile mtumishi wako alivyosema.”

36Mara alipomaliza kusema, wana wa mfalme wakaingia ndani wakiomboleza kwa makelele. Pia mfalme na watumishi wake wote wakalia sana kwa uchungu.

37Absalomu akakimbia na kwenda kwa Talmai mwana wa Amihudi, mfalme wa Geshuri. Lakini Mfalme Daudi akaomboleza kwa ajili ya mwanawe kila siku.

38Baada ya Absalomu kukimbia na kwenda Geshuri, akakaa huko miaka mitatu. 39Roho ya Mfalme Daudi ikatamani kumwendea Absalomu, kwa maana mfalme alikuwa amefarijika kuhusu kifo cha Amnoni.

Copyright information for Neno