2 Samuel 18
Kifo Cha Absalomu
1Daudi akakusanya watu aliokuwa nao na kuweka majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. 2Daudi akatuma vikosi vya askari: theluthi moja ilikuwa chini ya amri ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Mfalme akaviambia vikosi, “Hakika mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nanyi.”3Lakini watu wakasema, “Haikupasi kwenda, ikiwa sisi tutalazimika kukimbia, wao hawatatujali. Hata kama nusu yetu tukifa hawatajali, lakini wewe una thamani ya watu kama sisi kumi elfu. Ingekuwa bora zaidi kwako basi kutupatia msaada kutoka mjini.”
4Mfalme akajibu, “Nitafanya lo lote linaloonekana jema zaidi kwenu.”
Kwa hiyo mfalme akasimama kando ya lango wakati watu wote wakitoka nje kwa makundi ya mamia na maelfu. 5Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Iweni wapole kwa kijana Absalomu kwa ajili yangu.” Vikosi vyote vikasikia mfalme akitoa amri kwa kila jemadari kumhusu Absalomu.
6Jeshi likatoka kwenda kwenye uwanja wa vita kupigana na Israeli, hivyo vita vikapiganwa katika msitu wa Efraimu. 7Huko jeshi la Israeli likashindwa na watu wa Daudi, siku hiyo majeruhi walikuwa wengi kiasi cha watu ishirini elfu. 8Vita vikaenea nchi nzima, watu wengi zaidi wakifia msituni siku hiyo kuliko waliouawa kwa upanga.
9Basi ikawa Absalomu alikutana na watu wa Daudi. Yeye alikuwa amepanda nyumbu wake, naye nyumbu alipopita chini ya matawi yaliyosongana ya mwaloni mkubwa, kichwa cha Absalomu kilinaswa kwenye mti. Akaachwa ananing'inia hewani, wakati nyumbu aliyekuwa amempanda aliendelea kwenda.
10Mmojawapo wa wale watu alipoona, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akining'inia kwenye mti wa mwaloni.”
11Yoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo mpaka chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi ▼
▼18.11 Shekeli kumi za fedha ni sawa na gramu 115
za fedha na mkanda wa askari shujaa.”12Lakini huyo mtu akajibu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000 ▼
▼18.12 Shekeli 1,000 za fedha ni sawa na kilo 11.5
mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’ 13Nami kama ningekuwa nimemtendea kwa hila, na hakuna lo lote linalofichika kwa mfalme, wewe mwenyewe ungejitenga nami.”14Yoabu akasema, “Mimi sitapoteza muda hapa pamoja nawe.” Hivyo akachukua mikuki mitatu mkononi mwake na kumchoma nayo Absalomu kwenye moyo alipokuwa angali hai akiwa ananing'inia katika ule mwaloni. 15Nao wabeba silaha kumi wa Yoabu wakamzunguka Absalomu, wakampiga na kumwua.
16Kisha Yaobu akapiga tarumbeta, navyo vikosi vikaacha kuwafuata Israeli, kwa maana Yoabu aliwasimamisha. 17Wakamchukua Absalomu, wakamtupa katika shimo kubwa huko msituni na kulundika lundo kubwa la mawe juu yake. Huko nyuma, Waisraeli wote wakakimbilia nyumbani kwao.
18Wakati wa uhai wa Absalomu alikuwa amechukua nguzo na kuisimamisha katika Bonde la Mfalme, kwa maana alifikiri, “Sina mwana atakayeendeleza kumbukumbu ya jina langu.” Akaita nguzo hiyo kwa jina lake mwenyewe. Nayo inaitwa Mnara wa Ukumbusho wa Absalomu mpaka leo.
Daudi Aomboleza Kifo Cha Absalomu
19Basi Ahimaasi mwana wa Sadoki akasema, “Niruhusu mimi nikimbie na kumpelekea mfalme habari kwamba BWANA amemwokoa mfalme kutoka mikononi mwa adui zake.”20Yoabu akamwambia Ahimaasi, “Leo si wewe utakayepeleka habari. Unaweza kupeleka habari wakati mwingine, lakini leo haikupasi kupeleka, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.”
21Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja Mkushi, “Nenda, ukamwambie mfalme kile ulichoona.” Mkushi akasujudu mbele ya Yoabu akaondoka mbio.
22Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia tena Yoabu, “Liwalo na liwe, tafadhali niruhusu nikimbie nyuma ya huyo Mkushi.”
Lakini Yoabu akajibu, “Mwanangu, mbona wataka kwenda? Wewe huna habari yo yote itakayokupatia tuzo.”
23Ahimaasi akasema, “Liwalo na liwe, nataka kukimbia.”
Kwa hiyo Yaobu akamwambia, “Haya, kimbia!” Ndipo Ahimaasi akakimbia kufuata njia ya kupitia tambarare, akafika kabla ya huyo Mkushi.
24Wakati Daudi alipokuwa ameketi kati ya lango la ndani na la nje, mlinzi akapanda juu ya paa la lango kupitia ukutani. Alipotazama nje, akaona mtu mmoja akikimbia peke yake. 25Mlinzi akampazia mfalme sauti na kumpa taarifa.
Mfalme akasema, “Ikiwa yuko peke yake, lazima atakuwa na habari njema.” Naye yule mtu akazidi kusogea karibu.
26Kisha mlinzi akaona mtu mwingine anakuja akikimbia, akamwita bawabu, “Tazama, mtu mwingine anakuja akikimbia peke yake!”
Mfalme akasema, “Lazima atakuwa analeta habari njema pia.”
27Mlinzi akasema, “Ninaona kuwa yule wa kwanza anakimbia kama Ahimaasi mwana wa Sadoki.”
Mfalme akasema, “Yeye ni mtu mwema. Analeta habari njema.”
28Ndipo Ahimaasi akamwita mfalme, akasema, “Mambo yote ni mema!” Akasujudu mbele ya mfalme uso wake mpaka ardhini, akasema, “Ahimidiwe BWANA Mungu wako! Yeye aliyewatoa watu wale walioinua mikono yao dhidi ya mfalme bwana wangu.”
29Mfalme akauliza, “Je, huyo kijana Absalomu yuko salama?”
Ahimaasi akajibu, “Kulikuwa na machafuko mengi mara tu Yoabu alipokuwa anataka kumtuma mtumishi wa mfalme pamoja nami mtumishi wako, lakini sijui ilikuwa nini?”
30Mfalme akasema, “Simama kando na usubiri hapa.” Basi akasogea kando na kusimama hapo.
31Ndipo huyo Mkushi akawasili na kusema, “Mfalme bwana wangu, sikia habari njema! Leo BWANA amekuokoa kutoka kwa wale wote walioinuka dhidi yako.”
32Mfalme akamwuliza huyo Mkushi, “Je, kijana Absalomu yuko salama?”
Huyo Mkushi akajibu, “Adui wa mfalme bwana wangu na wote wale walioinuka kukudhuru na wawe kama huyo kijana.”
33Mfalme akatetemeka. Akapanda chumbani juu kupitia langoni akilia. Alipokuwa akienda, akasema, “Ee mwanangu Absalomu! Mwanangu, mwanangu Absalomu! Laiti ningekufa badala yako: Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”
Copyright information for
Neno