2 Thessalonians 3

Ombi La Kuhitaji Maombi

1Hatimaye, ndugu, tuombeeni ili kwamba Neno la Bwana lipate kuenea kwa haraka na kuheshimiwa kila mahali, kama vile ilivyokuwa kwa upande wenu. 2Ombeni pia ili kwamba tupate kuokolewa kutokana na watu waovu na wabaya, kwa maana si kila mmoja ana imani. 3Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawaimarisha ninyi na kuwalinda kutokana na yule mwovu. 4Nasi tuna tumaini katika Bwana ya kuwa mnafanya na mtaendelea kufanya yale tuliyowaagiza. 5Bwana aiongoze mioyo yenu katika upendo wa Mungu na katika saburi ya Kristo.

Onyo Dhidi Ya Uvivu

6Ndugu, tunawaagiza katika Jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni na kila ndugu ambaye ni mvivu na ambaye haishi kufuatana na maagizo tuliyowapa. 7Maana ninyi wenyewe mnajua jinsi iwapasavyo kufuata mfano wetu. Sisi hatukuwa wavivu tulipokuwa pamoja nanyi, 8wala hatukula chakula cha mtu ye yote pasipo kukilipia. Badala yake tulifanya kazi kwa bidii usiku na mchana, ili tusimlemee mtu ye yote miongoni mwenu. 9Tulifanya hivi, si kwa sababu hatukuwa na haki ya kupata msaada kama huo, lakini ili kusudi tujifanye sisi wenyewe kuwa kielelezo. 10Kwa maana hata tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwapa amri ili kwamba: “Mtu ye yote asiyetaka kufanya kazi, wala asile.”

11Kwa kuwa tunasikia kwamba baadhi ya watu miongoni mwenu ni wavivu. Hawafanyi kazi bali hujishughulisha na mambo ya wengine. 12Basi watu kama hao tunawaagiza na kuwaonya katika Jina la Bwana Yesu Kristo wafanye kazi kwa utulivu na kujipatia mahitaji ya maisha yao wao wenyewe. 13Kwa upande wenu, ndugu, ninyi kamwe msichoke katika kutenda mema.

14Ikiwa mtu ye yote hayatii maagizo yetu yaliyoko katika barua hii, mwangalieni sana mtu huyo. Msishirikiane naye, ili kwamba apate kuona aibu. 15Lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.

Salamu Za Mwisho

16Basi, Bwana wa amani mwenyewe awapeni amani nyakati zote na kwa kila njia. Bwana awe nanyi nyote.

17Mimi, Paulo, ninaandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndio alama ya utambulisho katika barua zangu zote. Hivi ndivyo niandikavyo.

18Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi nyote. Amen.

Copyright information for Neno