2 Timothy 2

Askari Mwema Wa Kristo Yesu

1Basi, wewe mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo ndani ya Kristo Yesu. 2Nayo mambo yale uliyonisikia nikiyasema mbele ya mashahidi wengi, uwakabidhi watu waaminifu watakaoweza kuwafundisha watu wengine vile vile. 3Vumilia taabu pamoja nasi kama askari mwema wa Kristo Yesu. 4Hakuna askari ye yote ambaye akiwa vitani hujishughulisha na mambo ya kawaida ya maisha haya kwa sababu nia yake ni kumpendeza yule aliyemwandika awe askari. 5Vivyo hivyo, yeye ashindanaye katika michezo hawezi kupewa tuzo ya ushindi asiposhindana kulingana na kanuni za mashindano. 6Mkulima mwenye bidii ya kazi ndiye anayestahili kuwa wa kwanza kupata fungu la mavuno. 7Fikiri sana kuhusu haya nisemayo, kwa maana Mungu atakupa ufahamu katika mambo hayo yote.

8Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka kutoka kwa wafu, yeye aliye wa uzao wa Daudi. Hii ndiyo Injili yangu, 9ambayo kwayo ninateseka hata kufikia hatua ya kufungwa minyororo kama mhalifu. Lakini neno la Mungu halifungwi. 10Kwa hiyo ninavumilia mambo yote kwa ajili ya wateule wa Mungu, kusudi wao nao wapate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.

11Hili ni neno la kuaminiwa: Kwa maana kama tumekufa pamoja naye,
tutaishi pia pamoja naye.
12Kama tukistahimili,
pia tutatawala pamoja naye.
Kama tukimkana yeye,
naye atatukana sisi.
13Kama tusipoamini,
yeye hudumu kuwa mwaminifu,
kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.


Mfanyakazi Aliyekubaliwa Na Mungu

14Endelea kuwakumbusha mambo haya ukiwaonya mbele za Bwana waache kushindana kwa maneno ambayo hayana faida yo yote bali huwaangamiza tu wale wanaoyasikia. 15Jitahidi kujionyesha kwa Mungu kuwa umekubaliwa naye, mtenda kazi asiye na sababu ya kuona aibu, ukilitumia kwa usahihi neno la kweli. 16Jiepushe na maneno mabaya, yasiyo na maana, yasiyo ya utauwa, kwa maana hayo huzidi kuwatosa watu katika kukosa heshima kwa Mungu. 17Mafundisho yao yataenea kama kidonda kisichopona. Miongoni mwao wamo Himenayo na Fileto 18ambao wameiacha kweli, wakisema kwamba ufufuo wa wafu umekwisha kuwako na kupotosha baadhi ya watu. 19Lakini msingi wa Mungu ulio madhubuti umesimama ukiwa na muhuri wenye maandishi haya: “Bwana anawajua walio wake” tena, “Kila alitajaye jina la Bwana auache uovu.”

20Katika nyumba kubwa si kwamba kuna vyombo vya dhahabu na fedha tu, bali pia vimo vyombo vya miti na vya udongo, vingine kwa matumizi maalum na vingine kwa matumizi ya kawaida. 21Basi ikiwa mtu amejitakasa na kujitenga na hayo niliyoyataja, atakuwa chombo maalum, kilichotengwa na ambacho kinamfaa mwenye nyumba, kimeandaliwa tayari kwa kila kazi njema.

22Zikimbie tamaa mbaya za ujana, ufuate haki, imani, upendo na amani pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi. 23Jiepushe na mabishano ya kipumbavu na yasiyo na maana, kwa kuwa wajua ya kwamba hayo huzaa magomvi. 24Tena haimpasi mtumishi wa Bwana kuwa mgomvi, bali inampasa awe mwema kwa kila mtu, awezaye kufundisha, tena mvumilivu. 25Inampasa kuwaonya kwa upole wale wanaopingana naye, kwa matumaini kwamba Mungu atawajalia kutubu na kuijua kweli, 26ili fahamu zao ziwarudie tena, nao waponyoke katika mtego wa ibilisi ambaye amewateka wapate kufanya mapenzi yake.

Copyright information for Neno