3 YOHANA

3 Yohana

Utangulizi

Waraka wa tatu wa Yohana uliandikiwa Gayo, ambaye alikuwa kiongozi muhimu katika kanisa. Anaelekezwa kuwasaidia na kuwahudumia wale wanaokuja kama wajumbe wa Mungu. Pia anapewa onyo kuhusu Deotrefe, juu ya tabia yake ya kukosa ushirikiano. Yohana anaeleza tarajio lake la kuja na kushughulikia tatizo hili yeye mwenyewe.Wazo Kuu

Wajibu binafsi wa Gayo kuhusu watumishi wa kweli na wa uongo.Mwandishi

Mtume Yohana.Kusudi

Yohana anamwandikia Gayo akimpa onyo kuhusu Deotrefe juu ya tabia yake ya kukosa ushirikiano.Mambo Muhimu

Yohana anamtakia Gayo kufanikiwa katika mambo yote, na pia anamwagiza asiige lililobaya bali lililo jema.Mahali

Efeso.Tarehe

Kama mwaka wa 90 B.K.Wahusika Wakuu

Yohana, Gayo, Deotrefe na Demetrio.Mgawanyo

  • • Salamu (1:1-4)
  • • Kutiwa moyo kwa Gayo (1:5-8)
  • • Kukemewa kwa Deotrefe (1:9-10)
  • • Kusifiwa kwa Demetrio (1:11-12)
  • • Hitimisho (1:13-15).

3 John

Salamu

1Mzee:

Kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli.

Gayo Anasifiwa Kwa Ajili Ya Ukarimu Wake

2Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo. 3Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza juu ya uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli. 4Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

5Mpenzi, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako. 6Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya kanisa. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu. 7Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wo wote kutoka kwa watu wasioamini. 8Kwa hiyo imetupasa sisi kuonyesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.

Deotrefe

9Nililiandikia kanisa, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu. 10Hivyo kama nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke kanisani.

Demetrio

11Mpenzi, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Ye yote atendaye mema atoka kwa Mungu, atendaye mabaya hakumwona Mungu.

12Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.

Salamu Za Mwisho

13Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino. 14Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.Amani iwe kwako. Rafiki zetu walioko hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walioko huko, kila mmoja kwa jina lake.

Copyright information for Neno