Acts 20

Paulo Apita Makedonia Na Uyunani

1Baada ya kumalizika kwa zile ghasia, Paulo aliwaita wanafunzi pamoja akawatia moyo, akawaaga, akaanza safari kwenda Makedonia. 2Alipopita katika sehemu zile, akinena na watu maneno mengi ya kuwatia moyo, ndipo hatimaye akawasili Uyunani, 3ambako alikaa kwa muda wa miezi mitatu. Alipokuwa anakaribia kuanza safari kwa njia ya bahari kwenda Shamu, kwa sababu Wayahudi walikuwa wamefanya shauri baya dhidi yake, aliamua kurudi kwa kupitia njia ya Makedonia. 4Paulo alikuwa amefuatana na Sopatro mwana wa Piro, Mberoya, Aristarko na Sekundo kutoka Thesalonike na Gayo, mtu wa Derbe, Timotheo pamoja na Tikiko na Trofimo kutoka sehemu ya Asia. 5Hawa watu walitutangulia wakaenda kutungojea Troa. 6Lakini sisi tukasafiri kwa njia ya bahari kwa siku tano kutoka Filipi baada ya siku za Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, nasi tukaungana na wengine huko Troa, ambako tulikaa kwa siku saba.

Eutiko Afufuliwa Huko Troa

7Siku ya kwanza ya juma tulikutana pamoja kwa ajili ya kumega mkate. Paulo akaongea na watu, naye kwa kuwa alikuwa amekusudia kuondoka kesho yake, aliendelea kuongea mpaka usiku wa manane. 8Kwenye chumba cha ghorofani walimokuwa wamekutania kulikuwa na taa nyingi. 9Kijana mmoja jina lake Eutiko, aliyekuwa amekaa dirishani, wakati Paulo alipokuwa akiendelea kuhubiri kwa muda mrefu, alipatwa na usingizi mzito, akaanguka kutoka ghorofa ya tatu, wakamwinua akiwa amekufa. 10Paulo akashuka chini, akajitupa juu ya yule kijana na kumkumbatia, akasema, “Msishtuke, uzima wake bado umo ndani yake.” 11Kisha Paulo akapanda tena ghorofani, akamega mkate na kula. Baada ya kuongea mpaka mapambazuko, akaondoka. 12Watu wakamrudisha yule kijana nyumbani akiwa hai nao wakafarijika sana.

Paulo Awaaga Wazee Wa Efeso

13Tukaingia melini tukasafiri kwa njia ya bahari mpaka Aso ambako ndiko tungempakia Paulo, alikuwa amepanga hivyo maana alitaka kufika kwa miguu. 14Alipotukuta huko Aso, tulimpakia melini tukasafiri wote mpaka Mitilene. 15Kutoka huko tuliendelea kwa njia ya bahari na kesho yake tukafika mahali panapokabili Kio. Siku iliyofuata tukavuka kwenda Samo na kesho yake tukawasili Mileto. 16Paulo alikuwa ameamua tusipitie Efeso ili asitumie muda mwingi huko sehemu za Asia, kwa sababu alikuwa anatamani kama ikiwezekana kufika Yerusalemu kabla ya siku ya Pentekoste.

17Paulo akiwa Mileto, akatuma ujumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kanisa waje wakutane naye. 18Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi katikati yenu muda wote tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia. 19Nilimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lo lote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

22“Nami sasa nimesukumwa na Roho, ninakwenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. 23Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. 24Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Yesu aliyonipa, yaani, kazi ya kuishuhudia injili ya neema ya Mungu.

25“Nami sasa najua ya kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu ninyi ambaye nimemhubiria Ufalme wa Mungu katika kwenda kwangu huko na huko, atakayeniona uso tena. 26Kwa hiyo nawaambieni leo hii kwamba sina hatia ya damu ya mtu awaye yote. 27Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. 28Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Lichungeni kanisa lake Mungu alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. 29Najua kwamba baada mimi kuondoka, mbwa mwitu wakali watakuja katikati yenu ambao hawatalihurumia kundi. 30Hata kutoka miongoni mwenu wenyewe watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. 31Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya, kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.

32“Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa. 33Sikutamani fedha wala dhahabu wala nguo ya mtu ye yote. 34Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35Katika kila jambo nililofanya, nimewaonyesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Yesu mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni baraka zaidi kutoa kuliko kupokea.’ ”

36Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba. 37Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu, 38Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye mpaka kwenye meli.

Copyright information for Neno